Featured Kitaifa

TAASISI NA WATENDAJI WA TAASISI ZA UMMA WAHAKIKISHE MAZINGIRA WEZESHI YA BIASHARA NA UWEKEZAJI.

Written by mzalendoeditor

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara – Viwanda na Biashara Dkt. Hashil Abdallah amezishauri Taasisi za umma pamoja na watendaji wake wanaotoa huduma kuhakikisha wanaweka mazingira bora ya biashara na uwekezaji ili kifikia malengo ya Serikali ya Awamu ya Sita na kuliwezesha Taifa kufikia uchumi wa Kati wa Juu.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Abdallah katika ufunguzi wa semina ya Wajumbe wa Baraza la Ushindani iliyofanyika Novemba mosi (1) 2022 katika ukumbi wa Chuo cha Uvuvi, Mbegani, Bagamoyo amesema mazingira bora na wezeshi ni muhimu katika kuvutia wawekezaji, kuendeleza viwanda na kufanya biashara nchini.

Dkt. Abdallah pia amewashauri Wajumbe wa Baraza hilo kuainisha Sheria, Kanuni na Taratibu zote zinazosimamia sekta ya uwekezaji na biashara zenye changamoto katika uwekaji wa mazingira wezeshi ya biashara na uwekwzaji nchini ili zifanyiwe maboresho ziwezw kuendana na mabadiliko ya ukuaji wa uchumi na zikidhi mahitaji.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Ushindani (FCT) Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu-Divisheni ya Kazi, Mhe. Salma Maghimbi amesema Baraza hilo litaendelea kutenda haki katika maamuzi yake kwa kuzingatia sheria, kanuni taratibu pamoja na ushahidi na udhibiti unaotolewa kwa lengo la kuendeleza biashara, kuvutia uwekezaji na hatimae kukuza uchumi wa Taifa.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani (FCC) Bw. William Erio amesema FCC inashirikiana na FCT katika kuliwezesha Baraza kufanya maamuzi ya kesi zinazowasilishwa kwa Baraza hilo kutoka Mamlaka za Udhibiti mbalimbali ili kuhakikisha biashara zinaendelea kwa kizingatia usawa katika ushindani wa soko.

Akitoa taarifa ya utendaji kazi mbele ya Mgeni Rasmi, Msajili wa FCT, Mhe. Renatus Rutatinisibwa amesema Baraza hilo linajukumu la kupokea, kusikiliza na kutolea maamuzi kesi mashauri ya rufaa yatokanayo na ushindani wa kibiashara na udhibiti wa soko kutoka FCC, EWURA, LATRA, TCAA, TCRA na PURA.

Aidha, amesema Baraza hilo limepewa hadhi ya Kimahakama ya utoaji haki kwenye masuala ya Ushindani Udhibiti wa Soko naKumlinda mlaji. Maamuzi ya kesi za rufaa na maombi yanayotolewa na Baraza hilo ni ya mwisho.

About the author

mzalendoeditor