Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza baada ya kukagua ujenzi wa Chuo cha VETA Uyui mkoani Tabora, Septemba 8, 2022. Kulia ni Mkuu wa mkoa w Tabora, Batilda Burian.
……………………….
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) Mkoa wa Tabora, Musa Chaulo kuwakamata watu wote wanaohusika na usimamizi wa ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) wilaya ya Uyui mkoani Tabora kwa tuhuma za ubadhilifu wa fedha za mradi huo.
Amechukua hatua hiyo baada ya kukagua mradi huo na kuonesha kutoridhika na gharama za ujenzi wa baadhi ya majengo ikiwemo kibanda cha mlinzi ambacho ujenzi wake umegharimu shilingi milioni 11. “Sitamvumilia yeyote atakayemuhujumu Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, watafutwe na wachukuliwe hatua.”
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Alhamisi, Septemba 8, 2022) baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa chuo cha VETA wilaya ya Uyui mkoani Tabora ambapo amesema hajaridhishwa na ujenzi wa chuo hicho ambacho majengo yake yanejengwa kwa gharama kubwa tofauti na uhalisia kwa kutumia mfumo wa nguvu kazi ya ndani (force account).
Mbali na ujenzi wa kibanda cha mlinzi, pia Waziri Mkuu ameonesha kutoridhishwa na ujenzi wa nyumba za watumishi chuoni hapo ambapo nyumba moja yenye uwezo wa kuchukua familia mbili inajengwa kwa gharama ya shilingi milioni 114 na tayari wameshatumia zaidi ya shilingi milioni 70 na bado haijakamilika.
“Nyumba moja yenye uwezo wa kuchukua familia tatu Wizara ya Afya inajenga kwa shilingi milioni 90 na Ofisi ya Rais (TAMISEMI) wanajenga nyumba za walimu zenye uwezo wa kuchukua familia mbili kwa gharama ya shilingi milioni 57 na wanajenga kwa mfumo wa force account kama mnavyojenga hapa, hii haikubaliki.”
Kutokana na kutoridhishwa na ujenzi wa chuo hicho unaosimamiwa na VETA, Mheshimiwa Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt. Batilda Burian asimamie ujenzi wa chuo hicho ili uweze kukamilika kwa wakati. “Mkuu wa mkoa simamia vizuri ujenzi wa chuo hiki, tunataka ukamilike kwa wakati.”
Mheshimiwa Majaliwa amesema ujenzi wa vyuo hivyo unatokana na maono mazuri ya Mheshimiwa Rais Samia kwa lengo la kuwawezesha vijana kupata ujuzi utakaowawezesha kujiajiri au kuajiriwa na hatimaye kupunguza changamoto ya ajira nchini. “…Kila siku Mkuu wa Nchi anawasisitiza Watanzania juu ya matumizi mazuri ya fedha za umma, waliohusika wote wachukuliwe hatua.”
Awali, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore alisema ujenzi huo unaotarajiwa kugharimu shilingi bilioni 2.9 unahusisha jumla ya majengo 17 ambayo ni jengo la utawala, majengo manne ya karakana, madarasa mawili makubwa, mabweni mawili, nyumba mbili za watumishi, jengo la umeme, jengo la bohari na jengo la ofisi ya mlinzi.
Alitaja fani zitakazokuwa zinatolewa baada ya kukamilika kwa chuo hicho ni uhazili na kompyuta, ubunifu wa mitindo, uashi, umeme wa majumbani, ufundi wa magari, uchomeleaji na uungaji vyuma, ufugaji wa samaki, matumizi ya kompyuta, usindikaji wa mazao ya nyuki, mapambo na kutengeneza bidhaa za batiki, kilimo cha mbogamboga na udereva.
Kibanda cha mlinzi katika Chuo cha VETA Uyui mkoani Tabora ambacho kimejengwa kwa gharama ya sh.milioni 11. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye alikagua ujenzi wa Chuo hicho, Septemba 8, 2022 aliagiza TAKUKURU iwakamate waliosimamia ujenzi huo.
Nyumba ya walimu wa Chuo cha VETA Uyui mkoani Tabora ambayo imekadiriwa kujengwa kwa sh, milioni 114 na hadi sasa imetumia zaidi ya milioni 70. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye alikagua ujenzi wa Chuo hicho Septemba 8, 2022 aliagiza Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora isimamie ujenzi huo ili kudhibiti gharama kubwa zinazotumika katika ujenzi huo.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza baada ya kukagua ujenzi wa Chuo cha VETA Uyui mkoani Tabora, Septemba 8, 2022. Kulia ni Mkuu wa mkoa w Tabora, Batilda Burian.
Muonekano wa hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa Chuo cha VETA Uyui mkoani Tabora. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alikagua ujenzi wake Septemba 8, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)