Featured Kitaifa

SERIKALI YAPIGA MARUFUKU WALIMU KUPITA KILA OFISI YA HALMASHAURI KUTAFUTA HUDUMA.

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Innocent Bashungwa,wakati akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Septemba 8,2022 jijini Dodoma kuhusu uboreshaji wa huduma kwa walimu nchini.

…………………

Na Alex Sonna-DODOMA

SERIKALI imepiga marufuku walimu kupita kila Ofisi ya halmashauri kutafuta huduma na kuwataka watoa huduma za walimu kuwafuata shuleni badala ya kukaa ofisini.

Hayo ameyasema leo Septemba 8,2022 Jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Innocent Bashungwa,wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uboreshaji wa huduma kwa walimu nchini.

Waziri Bashungwa amewataka watendaji wote wanaowahudumia walimu,wahakikishe wanakuwa karibu na walimu, wanasimamia kupokea kero na malalamiko ya walimu katika maeneo yao ya kazi na kuzitatua ipasavyo kwa wakati,

“Ni marufuku kuwaacha walimu kupita kila ofisi ya Halmashauri kutafuta huduma, narudia tena mwalimu apelekewe huduma shuleni badala ya watoa huduma kukaa ofisini” amesema Bashungwa

Bashungwa amesema kuwa Mwalimu akiandika barua kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhitaji huduma, anapaswa kujibiwa kwa maandishi ndani ya siku 7 baada ya kupokelewa.

Aidha, Bashungwa amewaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya zote nchini kuwasimamia Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, Maafisaelimu, Maafisa wa Tume ya Utumishi wa Walimu, Wathibiti Ubora wa Shule kuhakikisha wanawafuata walimu mashuleni na kutatua kero na malalamiko yao kwa wakati.

Amewataka viongozi hao kufuatilia na kuwasimamia viongozi wa elimu katika ngazi ya Mikoa, Halmashauri, Kata na shule kutekeleza mikakati ya uboreshaji na usimamizi wa elimu na kuhakikisha wanawasilisha taarifa ya utekelezaji Ofisi ya Rais – TAMISEMI kila robo mwaka.

Hata hivyo  amewataka kusimamia utekelezaji wa Mipango ya Mafunzo kazini kwa walimu, kwa mujibu wa Mwongozo uliotolewa na Katibu Mkuu Utumishi na ufanyike kwa uwazi na ushirishwaji wa kutosha, ili kuondoa dhana ya kuwa waajiri wanatoa nafasi za mafunzo kwa upendeleo.

Pia, Bashungwa amewaelekeza Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuwasimamia Maafisa wa Tume ya Utumishi wa Walimu kuzingatia miongozo ya upandishwaji vyeo walimu, ili kila anayestahili kupandishwa cheo, anapandishwa kwa mujibu Sheria, Kanuni na Miongozo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Innocent Bashungwa,wakati akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Septemba 8,2022 jijini Dodoma kuhusu uboreshaji wa huduma kwa walimu nchini.

About the author

mzalendoeditor