WAZIRI wa Maliasili na utalii Balozi Dkt Pindi Chana akiongea na waandishi wa habari baada ya kufungua mkutano wa nane wa kimataifa wa Wanasayansi wa mambo ya kale.
Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya mkutano wa nane wa kimataifa wa Wanasayansi wa mambo ya kale Profesa Jackson Njau ambaye pia ni muadhiri wa chuo kikuu cha Indiana Marekani akiongea na waandishi wa habari juu ya mkutano huo.
Dkt Charles Saanane akiongea na waandishi wa habari juu ya nyayo za kale zilizopo eneo la Laitoli ndani ya mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro.
BAADHI ya Wanasayansi watafiti wa mambo ya kale kutoka nchi mbalimbali wakiwa katika mkutano wao wa nane mkoani Arusha.
……………………………………..
NA NAMNYAK KIVUYO, ARUSHA
Waziri wa Maliasili na utalii Balozi Dkt Pindi Chana amesema kuwa katika bajeti ya wizara hiyo 2022/2023 wameweka mkakati wa kuboresha utunzaji na uhifadhi wa miundombinu ya malikale ili kuweza kuwavutia zaidi watalii kuja nchini.
Dkt Chana aliyasema hayo wakati akifungua mkutano wa nane wa kimataifa wa Wanasayansi wa mambo ya kale(EAAPP) ambapo alisema kuwaTanzania itaendelea kuwa hazina ya kuweka historia ya mali kale na masalia ya kale Afrika mashariki.
“Tutaendelea kutunza iwe ni sehemu ya historia na tafiti ambapo tunashirikiana na tasisi mbalimbali ikiwemo vyuo vikuu ambavyo vina kozi ya kufundisha masuala haya ya mali kale na masalia ya kale kwahiyo hiyo ni moja ya kipaumbele chetu kuona ni namna gani tunaweza kutunza na kuhifadhi ili watu waje kujifunza na kutalii,” Alisema Dkt Chana.
Alifafanua kuwa pia wameendelea kuweka taarifa vizuri katika Maktaba mbalimbali hususan katika vyuo vikuu pamoja na makumbusho yote yasiyo pungua saba ambayo wataendelea kutunza historia hiyo muhimu kwa faida ya kizazi hiki na kizazi kijacho.
Aidha alieleza kuwa mkutano huo ni moja ya muoendelezo ya programu ya Tanzania the Royal Tour ambao umewakutanisha washiriki takribani 100 kutoka katika nchi 10 ambao ni watafiti mbalimbali wa masuala ya masalia ya mali kale ambapo wataendelea kuwa na mazao mapya ya utalii kwani Tanzania ni Tanzania ni hazina ya masuala hayo.
Kwa upande wake Profesa kutoka Chuo Cha Indiana Marekani Prof: Jackson Njau ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya mkutano huo alieleza kuwa mkutano huo ni jumuiya ya wanataaluma wa mambo ya kale na jiolojia ambao wanafanya tafiti katika bonde la Ufa kwanzia Ethiopia, Kenya na Tanzania, ambapo Tanzania ina maeneo mengi ya zama za mali kale ambayo ni pamoja na Oduvai Gorge na Laitole.
Aliendelea kusema kuwa jumuiya hiyo ilianzishwa 2007 kwa lengo la kuwaleta pamoja watafiti, wahifadhi, walimu, wanafunzi, wasimamizi na watunga sera katika taaluma za Akiolojia, Paleontolojia na Jiolojia katika bonde la Ufa kujumuika na kubadishana mawazo juu ya matokeo ya tafiti zao.
“Jumuiya hii ni ya pekee na ya kwanza Afrika Mashariki kutokana na masalia yetu na historia yetu na tija kubwa ni kwamba Wanasayansi wa Afrika Mashariki inawapa fursa ya kuleta mikutano ambayo ni rahisi kuhudhuria wanazuoni wa Kiafrika kutokana na Jumuiya kubwa mikutano yake kufanyika Marekani ambayo ni gharama kubwa hali iliyokuwa ikipelekea wengi kutohudhiria ingawa mikusanyo inayoripotiwa inatoka kwetu,” Alisema Profesa Njau.
Alifafanua kuwa kwa miaka takriban 16 EAAPP imeendelea kuwa kiungo muhimu cha kuwaelimisha wajumbe wake kuhusu matokeo ya tafiti mbalimbali zinazofanyika katika Bonde la Ufa ambalo ndilo chimbuko kuu la mwanadamu ambapo mpaka Sasa jumuiya hiyo ina wanachama 150.
Naye mwanazuoni Dkt Charles Saanane ambaye pia amefanya tafiti nyingi takriban miaka 40 hususan eneo la Olduvai alieleza kuwa nyayo za Laitole zina karibu miaka milioni 3 ambapo nyayo hizo zimehifadhiwa kwa kuzikwa baada ya kufanya majaribio ambayo yalioneka kuwa kuzibeba nyayo hizo zitaaharibika ambapo unatakiwa utafiti mzuri wa kuweza kuandaa viifadhiwe hapohapo.