MKURUGENZI wa taasisi ya Saratani Ocean road Dkt Julius Mwaisilage wakati akisoma hotuba ya waziri wa Afya Ummy Mwalimu katika ufunguzi kongamano la kwanza la kimataifa la Saratani linaloendelea mkoani Arusha.
Rais wachama cha madaktari bingwa wa maradhi ya Saratani(TOS) Dkt Jerry Ndumbaro akiongea na waandishi wa habari mara baada ya kufunguliwa kwa kongamano la kwanza la kimataifa la Saratani linaloendelea mkoani Arusha.
BAADHI ya wataalamu na wadau wa ugonjwa wa Saratani wakiwemo madaktari wakifuatilia kongamano la kwanza la kimataifa la Saratani lililofanyika mkoani Arusha.
…………………………………..
NA NAMNYAK KIVUYO, ARUSHA.
Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amekitaka chama cha madaktari bingwa wa maradhi ya Saratani(TOS) kuhamasisha madaktari waliomaliza masomo na wanaofanya kazi kujiunga katika kusomea programu ya Saratani(oncology) ili kuweza kuondokana upungufu wa madaktari bingwa wa Saratani ambao mpaka sasa wapo 38 nchi nzima.
Rai hiyo imetolewa na mkurugenzi wa taasisi ya Saratani Ocean road Dkt Julius Mwaisilage wakati akisoma hotuba ya waziri wa Afya Ummy Mwalimu katika ufunguzi kongamano la kwanza la kimataifa la Saratani lilijumisha wataalamu na wadau ambapo alisema kuwa kutokana na upungufu mkubwa wa madaktari bingwa wa Saratani daktari mmoja kwa mwaka anahudumia wagonjwa 1200.
Dkt Mwaisilage alisema kama chama wana malengo yao lakini kikubwa wahamasishe wataalamu waweze kusomea kwani serikali inatoa ufadhili kila mwaka kwa kupeleka fedha chuo kikuu cha Afya na sayansi shirikishi Muhimbili(MUHAS) hivyo wawahamasishe ili kupunguza upungufu huo.
Aidha alisema kuwa kulingana na takwimu wanazoziona katika hosipitali kwa mwaka wanawaona wagonjwa 14600 sawa na asilimia 33 ambapo idadi hiyo ni ndogo kwani Tanzania ina zaidi ya wagonjwa elfu 42 wa Saratani.
Sambamba na hayo alisema kuwa serikali imejipanga katika kuhakikisha wanaboresha miundombinu ya kutibu ugonjwa wa saratani ikiwemo tiba ya upasuaji na uchunguzi wa ugonjwa huo katika hospitali zote za kanda na taifa nchini.
“Lengo ni kuhakikisha wagonjwa wote wanachunguzwa na wanapatiwa tiba ya upasuaji lakini kwa upande wa mionzi serikali inaendelea na kuboresha katika sehemu nyingine kwani kwa sasa zinapatika katika hospitali ya Bugando na Taasisi ya saratani ya Ocean road,”Alisema.
Alisema tiba ya mionzi inaendelea kuboreshwa nchini ikiwa sasa wanaendelea katika hospitali ya KCMC pamoja na Benjamin Mkapa ikifuatiwa na Mbeya lengo ni kuhakikisha huduma za utambuzi wa saratani zinawafikia wananchi katika kanda zote.
Kwa upande wake Rais wa TOS Dkt Jerry Ndumbaro alisema lengo la kongamano hilo la kimataifa ni kubadilishana uzoefu wa kisayansi katika kuboresha huduma kwani ugonjwa wa saratani umekuwa ukiongezeka kwa wingi na kufanya idadi ya wagonjwa kuwa kubwa ambapo katika takwimu za mwaka jana wagonjwa zaidi ya elfu 42 wanapatikana kwa mwaka ambapo lengo la kongamano hilo ni kubadilishana utaalam kwa wataalam wa ndani na nje ya Tanzania ili kuboresha huduma katika eneo la saratani.
“Mpango wetu ni kuwafikia watumishi wa afya nchi nzima walioko katika ngazi ya mkoa na wilaya katika kuwawezesha wataalamu kugundua ugonjwa huo mapema ili wagonjwa waweze kutibiwa,”alisema Dk.Ndumbaro.
Alisema kupitia chama hicho wanampango mkakati wa kufanya huduma za upimaji na ugunduzi wa mapema wa saratani katika jamii ambapo watapita kila mkoa kuhakikisha huduma hiyo inawafikiwa wananchi wa ngazi zote.
Alieleza kuwa chama kinahakikisha wanawawezesha wataalam na watoa huduma za afya ngazi za mikoa na wilaya kupata utaalam wa kuweza kugundua magonjwa hayo mapema na kutoa matibabu kwa wagonjwa ambapo mpango walionao ni kufanya huduma za upimaji na ugunduzi wa mapema wa saratani katika jamii.
Aliongeza kwa kueleza kuwa tafiti zinaonyesha kuwa mitindo ya maisha ikiwemo kutokufanya mazoezi,uzito uliopitiliza,ulaji mbaya wa vyakula,ni miongoni mwa dalili hatarishi za uwepo wa magonjwa wa saratani ambapo ameitaka jamii kuhakikisha inabadili mitindo ya maisha yao ili kuweza kujikinga na saratani.