Na Eleuteri Mangi, WUSM Dar es salaam
Serikali kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kwa kushirikiana na wasanii wa kike wa muziki nchini chini ya Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Dada Hood inayojishughulisha na kupinga unyanyasaji wa kijinsia na kuendeleza sanaa wameandaa Tamasha la kuichangia Timu ya Taifa ya wanawake “Twiga Stars,” katika kusherehekea Siku ya Wanawake Duniani Machi 8, 2022.
Akizungumza na waandishi wa habari Februari 23, 2022 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji na Mwanzilishi wa taasisi hiyo Mkuwe Issale (Mammy Baby) katika mkutano wa pamoja na Kaimu Katibu Mtendaji wa BMT, Neema Msitha, amesema tamasha hilo litafanyika Machi 8, 2022 katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC).
“Siku hiyo tumeipanga makusudi kwa kazi tatu ambazo ni kufanya harambee kuichangia timu ya wanawake Twiga Stars, kuzindua albamu yenye nyimbo za wasanii wa kike nchini ‘The Orange’ na kuonesha vipaji vya wanawake katika tasnia ya muziki” amesema Mkuwe.
Aidha, Mkurugenzi huyo amesema taasisi yake imekuja na ubunifu huo kwani inaunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwenye sekta za Sanaa na Michezo na juhudi za kupigania usawa wa jinsia.
Tamasha hilo litapambwa na burudani ya wasanii wa kike zaidi ya 10.
Kwa upande wake Kaimu Katibu Mtendaji wa BMT, Neema Msitha amewapongeza Dada Hood kwa kazi zao za kuwainua watoto wa kike hasa nia yao ya kuichangia timu ya wanawake ya Taifa Twiga Stars.
Neema ametoa wito kwa Watanzania kujitokeza kwa wingi siku hiyo ili kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kusaidia sekta ya michezo kwa upande wa timu za taifa za wanawake ambazo zinaendelea kupeperusha vema bendera ya taifa kimataifa.
Naye Kaimu Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Sanaa, Bi Leah Kihimbi amesema Rais Samia anapenda Sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo na taasisi ya Dada Hood ndiyo wamefungua milango ya mashirikiano na sekta binafsi na Serikali kwenye sekta za Sanaa na Michezo na kuzitaka taasisi nyingine kuiga mfano huo kwa maslahi mapana ya taifa.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chama cha Mpira wa Miguu Wanawake (TWFA), Somoe Ng’itu ameishukuru Serikali kwa kushirikiana na Taasisi ya Dada Hood na kuwakaribisha wadau wengine kuendelea kuwashika mkono Twiga Stars kwa niaba ya mabinti wengine michezoni kwani wanafanya vyema sana kimataifa ili waendelee kuliheshimisha Taifa.
Katika kikao hicho na waandishi wa habari, Taasisi ya Dada Hood pia imesaini Mkataba wa kusambaza album ya The Orange na kampuni ya Slide Visual ambapo sehemu ya mapato yatakayopatikana na yale ya harambee yatasaidia juhudi ya kupigania usawa wa jinsia, kuondoa ukatili kwa wanawake na kusaidia Twiga Stars.