Featured Kitaifa

MAKAMU WA RAIS AFUNGUA WARSHA YA UTUNZAJI WA BAHARI

Written by mzalendoeditor

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Amos Makala, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Selemani Jafo, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Dkt. Switbert Mkama, pamoja na Balozi wa kudumu wa Tanzania Umoja wa Mataifa New York Prof Kennedy Gastorn wakati alipowasili Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere Dar es salaam kufungua Warsha ya Umoja wa Mataifa kuhusu tathmini ya usimamizi wa mazingira ya Bahari

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwasili katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere uliopo Jijini Dar es salaam kufungua Warsha ya Umoja wa Mataifa kuhusu tathmini ya usimamizi wa mazingira ya Bahari

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akizungumza na washiriki wakati akifungua Warsha ya Umoja wa Mataifa kuhusu tathmini ya usimamizi wa mazingira ya Bahari inayofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere uliopo Jijini Dar es salaam

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiagana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Selemani Jafo (Kushoto) pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Amos Makala (Kulia) wakati akiondoka katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere uliopo Jijini Dar es salaam mara baada ya kufungua Warsha ya Umoja wa Mataifa kuhusu tathmini ya usimamizi wa mazingira ya Bahari

…………………………

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa. Dkt. Philip Mpango leo tarehe 19 Julai 2022 amefungua warsha ya Umoja wa Mataifa kuhusu tathmini, usimamizi na utunzaji wa mazingira ya Bahari, warsha inayofanyika katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es salaam kuanzia leo tarehe 19 hadi 27 Julai 2022.

Akizungumza na Viongozi na washiriki wa Warsha hiyo Makamu wa Rais amesema umoja baina ya mataifa pamoja na kujitolea ni mambo muhimu yatakayopelekea matumizi endelevu ya rasilimali za bahari pamoja na kuepusha kupotea kwa rasilimali hizo. Amesema ni lazima kuzuia na kupunguza uchafuzi wa bahari kwa kila namna kuanzia vyanzo vya ardhini hadi baharini. Ameongeza kwamba unahitajika muongozo endelevu wa biashara ili uchumi wa bahari uendane na mazingira ya baharini.

Pia Makamu wa Rais amesema kwa sasa katika kulinda bahari vinahitajika vitendo zaidi vitakavyokwenda sambamba na sayansi, uvumbuzi na teknolojia pamoja na ushirikishwaji wa wadau wote unaojumuisha vijana na wanawake katika mijadala ambao ni sehemu ya suluhu.

Halikadhalika Makamu wa Rais amesisitiza kwamba Tanzania imeendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kulinda mazingira ikiwemo mazingira ya bahari kama vile kupiga marufuku utumiaji wa mifuko ya plastiki inayotumika mara moja , kutenga asilimia 6.5 eneo la Bahari ya Hindi kuwa eneo tengefu la bahari, kudhibiti kwa asilimia 99 uvuvi haramu pamoja na kuimarisha ufuatiliaji wa shughuli za uvuvi wa bahari kuu.

Amesema umefika wakati wa kutafuta njia sahihi za kudhibiti na kusimamia shughuli zinazofanyika baharini, pamoja na namna bora ya kuweka uwiano wa kiuchumi, kijamii na kimazingira wakati wa kutumia rasilimali za bahari.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mheshimiwa Selemani Jafo amesema warsha hiyo imelenga kutambua mahitaji ya serikali katika kufanya tathmini ya mazingira ya bahari ikiwemo shughuli za kiuchumi, kuongeza uelewa wa matumizi sahihi ya bahari pamoja na kuvutia jamii ya wanasayansi katika kuandika tathmini kwa lengo la kuimarisha sera za kisayansi kwa utunzaji bora wa bahari na rasilimali zake na kuhakikisha uchumi wa buluu ni endelevu na wenye manufaa.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Dkt. Aboud Jumbe amesema kinachohitajika ni kuendelea kufanya kazi pamoja kitaifa, kikanda na kimataifa ikiwa pamoja na kuwashirikisha wadau, watumiaji wa bahari pamoja na jamii inayoishi pembezoni mwa bahari kwaajili ya kuwawezesha kiuchumi kwa kutumia uchumi wa buluu. Ameongeza kwamba Wataalam wanapaswa kuzingatia mahitaji ya watumiaji wa bahari ambao wanaishi pembezoni kwa kuwa wamebeba wajibu wa ulinzi wa rasilimali za baharini.

Awali mwakilishi wa Umoja wa Mataifa, kitengo cha mambo ya Bahari na Sheria za Kimataifa za Bahari Bi. Alice Hicuburundi amesema kwamba uelewa ni jambo muhimu zaidi katika kulinda, kuhifadhi na matumizi endelevu ya bahari. Amesema matumizi ya sayansi na teknolojia yakiungana na uelewa ndio yanapaswa kuwa msingi wa ulinzi na utawala wa bahari kwa maendeleo endelevu hasa katika kufikia lengo la 14 la Umoja wa Mataifa.
Madhumuni ya warsha hiyo ni kuwajengea uwezo washiriki juu ya usimamizi wa bahari ikiwemo kuonesha hali na mwelekeo wa bahari, vihatarishi vikuu vinavyoikabili bahari na mazingira yake, matokeo ya vihatarishi hivyo, na hatua mbalimbali za kupunguza athari hizo.

About the author

mzalendoeditor