Featured Kitaifa

WAZIRI NAPE:’TUNABORESHA MAZINGIRA YA WANAHABARI’

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Nnauye akifungua Mkutano wa Serikali na Wadau Kujadili kuhusu Maendeleo Endelevu ya Vyombo vya Habari Nchini, Mkutano huo Umefanyika leo Julai 13,2022 Jijini Dar es Salaam 

****************************

-Asema mapitio ya Sheria,Sera za Habari yanaendelea

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Mosses Nnauye amesema Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kuboresha mazingira ya Wanahabari na upatikanaji wa taarifa nchini katika mazingira yote.

Amesema ili kuhakikisha mazingira hayo yanaimarika, tayari mchakato wa kupitia Sheria, Kanuni na Sera ya Habari umeanza na unaendelea vizuri.

Ameyasema hayo wakati alifungua mkutano wa Serikali na Wadau uliokuwa ukijadili Maendeleo Endelevu ya Vyombo vya Habari Nchini Tanzania uliofanyika Julai 13, 2022 Jijini Dar es Salaam.

“Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 ilipotungwa ililenga kutatua changamoto mbalimbali Katika sekta ya habari ikiwemo ajira, maslahi, mazingira ya kazi na wajibu wao, Serikali imetoa nafasi kwa Wanahabari kuleta mbadala wa yale yanayolalamikiwa na Wanahabari ili kuyaboresha, lengo la mchakato wa maboresho ya Sheria ya Huduma za Habari ni kutunga sheria itakayodumu kwa muda mrefu” Amesema Waziri Nape.

Amesema Wizara anayoiongoza kwa kishirikiana na wadau wameanza kupitia na kuangalia Uhuru wa Vyombo vya Habari na upatikanaji wa Habari nchini na kwamba wamezungumza namna ambavyo teknolojia inashiriki kusaidia upatikanaji wa habari.

“Pia tumezungumza kuhusu Uhuru wa mazingira ya Wanahabari kufanya kazi vizuri, pamoja na maslahi yao, haya yote ni mambo ya muhimu sana katika tasnia hii muhimu katika nchi yetu” Amesema Waziri Nape.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Ofisi ya Dar es Salaam Bw. Michael Toto amesema Shirika hilo linaendelea kusaidia Wanahabari na Wafanyakazi wa vyombo vya habari kila mahali na huu ni mwaka wa kumi sasa tangu walipoanza shughuli hizo Nchini ambapo kwa sasa wanapitia Mpango wa Utekelezaji wa Umoja wa Mataifa-UN kuhusu Usalama wa Wanahabari, ili kuwalinda wafanyakazi wa vyombo vya habari na kukomesha kutokujali kwa uhalifu unaofanywa dhidi yao.

“Katika Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, na kupitia majukwaa mengine ya mazungumzo kama vile Siku ya Redio duniani na Siku ya Kimataifa ya Kukomesha Uhalifu dhidi ya Waandishi wa Habari, tunaheshimu kazi muhimu ya vyombo vya habari katika kujenga taasisi na jamii imara, vyombo vya habari na habari hutuleta pamoja ili kujifunza, kuelewa wengine, kusikia na kusikilizwa kuhusu masuala yanayohusu maisha yetu ya kila siku” Amesema Bw. Michael Toto.

Nae Balozi wa Switzerland Nchini Didier Chassot amesema nchi yake imekuwa ikishirikiana na sekta ya vyombo vya habari nchini kwa zaidi ya muongo mmoja na kwamba kwa sasa wanafanya kazi na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambacho kinatoa Kitabu cha Mwaka cha Ripoti ya Ubora wa Vyombo vya Habari.

Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO Bw. Verson Msigwa amesema mkutano huo ni muhimu kwa sababu una lengo la kuboresha uratibu wa hatua za wadau mbalimbali katika kuendeleza maendeleo ya vyombo vya habari, uhuru wa kujieleza, upatikanaji wa habari na mabadiliko ya kidijitali nchini.

About the author

mzalendoeditor