Featured Kitaifa

WATU WAWILI WANAOHIFADHI VITU VYA WIZI KATIKA GETO LAO WAKAMATWA

Written by mzalendoeditor

Na John Walter-Manyara

Polisi mkoani Manyara wanadai kuwakamata wanaume wawili John Lapia (31) fundi Pikipiki mkazi wa mtaa wa Maisaka mjini Babati na Philimon Bura (18) mkazi wa kijiji cha Bermi Babati wakiwa na mali zinazozaniwa kuwa ni za wizi pamoja na funguo bandia (master key) 117.

Jeshi hilo mkoani Manyara lipo katika operesheni mbalimbali za kukabiliana na uhalifu wa makosa makubwa na madogo ambayo yamekuwa kero kwa jamii katika mkoa huo ambapo wamefanikiwa kuwakamata watuhumiwa saba kwa nyakati tofauti.

Mbali na funguo hizo Polisi walibaini kuwa watu hao walikuwa na vitu vingine kama Mitungi minne ya Gesi, Sola Pannel Moja kampuni ya Sundar,Jiko moja la gesi la mafiga mawili (Plate 2), Mabati 17, Kava mbili za kiti cha Pikipiki,Fremu moja ya Pikipiki aina ya Kinglion, vifaa mbalimbali vya umeme,TV moja aina ya Zune,Jokofu moja aina ya Boss,Feni moja aina ya Dolphin,Radio moja Subwoofer,nyaya mita kumi, betri moja ya pikipiki,viti vitano vya Plastiki na dish moja la DSTV rangi ya bluu.

Akizungumza  leo Februari 22, 2022  kamanda wa polisi mkoani hapa, Benjamin Kuzaga amesema watu watu hao  walikamatwa Februari 20,2022  saa 14:00 mchana mtaa wa Maisaka B kata ya Maisaka na taratibu za kuwafikisha mahakamani zinaendelea.

Katika tukio jingine jeshi hilo linamshikilia Mohamed Kadali (42) mkazi wa Dar es salaam kwa kosa la kusafirisha madawa ya kulevya aina ya Mirungi bunda 110 sawa na kilo 45 akitumia gari yenye usajili namba T.892 DRQ na Tela lake lenye namba T 760 DRS.

Aidha kamanda Kuzaga amesema wanamshikilia Simango Kibindia (40) mkazi wa Enguero Sidani wilaya ya Kiteto kwa kumiliki silaha aina ya gobore kinyume na taratibu.

Kwa upande mwingine Kuzaga amewaambia waandishi wa habari kuwa wamemkamata John Maganga (24) mkazi wa Gabido kata ya Narri tarafa ya Bashnet wilaya ya Babati kwa madai ya kukutwa na pombe haramu (gongo) lita 220 iliyokuwa imehifadhiuwa kwenye madumu 11 yenye ujazo wa lita 20.

Jeshi hilo limeendelea kuwakumbusha wananchi kuendelea kushirikiana na polisi kutoa taarifa mbalimbali za kihalifu na uhalifu ili zishughulikiwe na kuhakikisha kuwa mkoa wa Manyara unakuwa salama.

About the author

mzalendoeditor