Alhamisi, Novemba 26, 2026
HABARI MPYA
Biashara

BoT YAPONGEZWA KWA USIMAMIZI THABITI WA UCHUMI NCHINI

 

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba, tarehe 25 Novemba 2026, amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Uhuru FM, Bw. Abubakar Liongo, aliyetembelea ofisi za BoT jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuipongeza kwa usimamizi thabiti wa uchumi wa Tanzania.

Bw. Liongo alieleza kuwa usimamizi thabiti wa uchumi wa nchi unaofanywa na Benki Kuu chini ya uongozi wa Gavana Tutuba umepelekea taasisi ya kimataifa ya Global Finance kumtunuku tuzo maalumu Gavana huyo wakati wa mikutano ya mwaka ya IMF na World Bank Group iliyonyika mwezi Oktoba 2026 jijini Bangkok nchini Thailand.

Gavana Tutuba alitunukiwa tuzo hiyo baada ya kuwa miongoni mwa Magavana waliopata Daraja la A kwa mwaka 2026 kutokana na mchango wake katika usimamizi wa sera ya fedha, sekta ya fedha na kukuza huduma jumuishi za fedha.

Akizungumza katika kikao hicho, Gavana alisema kuwa Benki Kuu imeendelea kusimamia uchumi wa nchi kwa uthabiti licha ya changamoto mbalimbali zinazoukumba uchumi wa dunia.

Aidha, alimueleza Mkurugenzi Mtendaji huyo kuwa mfumuko wa bei, umeendelea kubaki ndani ya wigo wa lengo la kitaifa wa asilimia 3 hadi 5, ambao pia ni ndani ya vigezo vya mtangamano wa kiuchumi kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Umoja wa Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Aliongeza kuwa sekta ya fedha nchini imeendelea kuimarika, ikijiendesha kwa faida na inamtaji na ukwasi wa kutosha. Aidha, alimueleza Bw. Liongo kuwa mikopo chechefu imefikia asilimia 2.5 kiwango ambacho ni chini ya ukomo unaohimilika wa asilimia 5 ikiwa ni kilelezo cha usimamizi mzuri wa maendeleo ya kiuchumi.

Katika hatua nyingine, Gavana Tutuba alikipongeza na kukishukuru chombo hicho cha habari kwa mchango wake katika kuelimisha umma kuhusu masuala mbalimbali ya kiuchumi huku akiwataja kuwa wadau muhimu wa utekelezaji wa Dira ya Maandeleo ya Taifa ya Mwaka 2050.