Jumatano, Novemba 25, 2026
HABARI MPYA
Kitaifa

WHI YAUZA NYUMBA ZENYE THAMANI YA ZAIDI YA SHILINGI BILIONI 2 MWANZA

 

Watumishi Housing Investments (WHI) imeingia mkataba wa mauzo ya nyumba 36 zenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 2 na kampuni ya The Big Best Company Ltd, inayojishughulisha na shughuli za uvuvi na uchakataji wa samaki mkoani Mwanza.

Mkataba huo umesainiwa leo, tarehe 25 Novemba, 2026, jijini Mwanza, na kuhitimisha mauzo ya nyumba zote 59 zilizojengwa na WHI katika mradi wa nyumba wa Kisesa.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa WHI, Arch. Sephania Solomon, amesema kuwa mauzo hayo ni hatua muhimu katika utekelezaji wa majukumu ya WHI ambayo ni kuhakikisha watumishi wa umma na wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii wanapata makazi bora.

Aidha, ameeleza kuwa ushirikiano huo unafungua fursa zaidi kwa WHI kushirikiana na sekta binafsi ambazo wafanyakazi wake ni wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii kuona ni namna gani wanaweza kukidhi mahitaji ya makazi na kuboresha ustawi kwa wafanyakazi wao

Makabidhiano ya nyumba hizo kwa kampuni ya The Big Best Company Ltd yatafanyika kwa mujibu wa makubaliano ya mkataba.

Kukamilika kwa mauzo ya nyumba zote 59 katika mradi wa Kisesa ni mafanikio mengine kwa WHI katika kuendeleza sekta ya makazi nchini, sambamba na kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.