Na Mwandishi Wetu
IRAN imesisitiza kuwa haitarejea katika mazungumzo na Marekani kwa lengo la kumaliza mzozo unaoendelea Mashariki ya Kati hadi masharti saba iliyoweka yatakapotekelezwa, hatua inayozidisha sintofahamu kuhusu juhudi za kidiplomasia za kurejesha amani katika eneo hilo.
Spika wa Bunge la Iran na kiongozi wa ujumbe wa nchi hiyo katika mazungumzo ya kutafuta suluhu ya mzozo kati ya Marekani, Israel na Iran, Mohammad Bagher Qalibaf, amesema Tehran haitakuwa tayari kuzungumza na Washington hadi masharti hayo yatimizwe.
Akizungumza kupitia televisheni ya taifa ya Iran, Qalibaf amesema nchi hiyo haitashiriki mazungumzo yoyote na Marekani kabla ya kutekelezwa kwa matakwa yake, huku akionya kuwa Iran inaweza kupanua wigo wa mapambano endapo itahisi kuchokozwa na wapinzani wake.
Ingawa serikali ya Iran haijaweka hadharani orodha kamili ya masharti hayo saba, vyombo vya habari vya taifa hilo vimeripoti kuwa baadhi yake ni kuondolewa kwa vikwazo vya kiuchumi, kusitishwa kwa mzingiro wa majini wa Marekani dhidi ya bandari za Iran na kurejeshwa kwa mali za nchi hiyo zilizozuiliwa nje ya mipaka yake.
Kauli hiyo imekuja wakati mvutano katika Mlango Bahari wa Hormuz ukiendelea kuongezeka, baada ya Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran (IRGC) kudai kuwa meli tatu za mafuta ziligonga mabomu ya majini na kushika moto baada ya kukiuka taratibu za kupita katika njia hiyo muhimu ya kimataifa.
Kwa mujibu wa madai ya kikosi hicho, meli hizo zilikumbwa na tukio hilo licha ya kuwa zinasindikizwa na kulindwa na ndege za kijeshi za Marekani. Hata hivyo, madai hayo yametolewa na upande wa Iran.
ISRAEL YAENDELEA NA MASHAMBULIZI GAZA
Wakati mvutano kati ya Iran na Marekani ukiendelea, hali ya usalama katika Ukanda wa Gaza imeendelea kuwa tete baada ya mashambulizi ya Israel yaliyofanyika usiku wa Jumatatu na alfajiri ya Jumanne kuripotiwa kuua takribani Wapalestina tisa, kwa mujibu wa taarifa za maafisa wa eneo hilo.
Miongoni mwa waliouawa ni Na’im Abu Nahl, aliyekuwa mkuu wa kitengo cha usalama wa ndani katika Wizara ya Mambo ya Ndani inayoongozwa na Hamas.
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amethibitisha kuuawa kwa kiongozi huyo na kusisitiza kuwa nchi yake itaendelea kulenga miundombinu na vikosi vya usalama vya Hamas.
Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya ya Gaza, zaidi ya Wapalestina 74,700 wameuawa tangu kuanza kwa vita kati ya Israel na Hamas, huku mapigano na mashambulizi yakiendelea kuongeza changamoto za kiusalama na kibinadamu katika eneo hilo.
Mchanganyiko wa mvutano kati ya Iran na Marekani, pamoja na kuendelea kwa mashambulizi ya Israel katika Ukanda wa Gaza, unaendeleza hali ya kutokuwa na uhakika kuhusu juhudi za kurejesha utulivu katika Mashariki ya Kati.


