Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta na Gesi, Dkt. James Mataragio, amesema Serikali inalenga kuongeza uwezo wa uzalishaji wa umeme nchini kufikia Megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030, ambapo Megawati 1,892 zinatarajiwa kuzalishwa kupitia vyanzo mbalimbali vya nishati jadidifu kama vile jua, biomasi, upepo n.k
Ameyabainisha hayo leo Novemba 12, 2026, jijini Dar es Salaam wakati akifungua Kongamano la Wiki ya Nishati Jadidifu 2026.
Ameeleza kuwa kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Tanzania inalenga kufikia uwezo wa kuzalisha umeme kwa kiasi cha Gigawati 70 ifikapo mwaka 2050 hivyo malengo hayo yanahitaji uwekezaji mkubwa, matumizi ya teknolojia bunifu na ushirikiano wa kimkakati kati ya Serikali, sekta binafsi na washirika wa maendeleo.
Amesema kwa sasa uwezo wa mitambo ya kuzalisha umeme nchini ni megawati 4,667.19 zinazotokana na vyanzo mbalimbali kama vile maji (2,726.34 MW), Gesi Asilia (1,281.19 MW), Biomasi (171.19 MW), Jua (99.44MW), Makaa ya mawe (45.40 MW), Upepo (3.90 MW) n.k.
Akizungumzia baadhi ya miradi ya nishati jadidifu, Dkt. Mataragio amesema Serikali inaendelea kutekeleza mradi wa umeme jua wa Megawati 150 katika Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, ambao tayari unachangia Megawati 50 kwenye Gridi ya Taifa baada ya kukamilika kwa Awamu ya Kwanza, huku Megawati 100 zilizobaki zikitarajiwa kuanza kuingizwa kwenye gridi mwaka 2027.
Ameongeza kuwa mradi wa umeme jua wa Zuzu mkoani Dodoma wenye uwezo wa Megawati 130 upo katika hatua za manunuzi, huku miradi mingine ya nishati ya jua, upepo na jotoardhi ikiendelea katika hatua mbalimbali za maandalizi.
Aidha, amesema Serikali inaendelea kutekeleza Mkakati wa Taifa wa matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia wa mwaka 2024–2034, wenye lengo la kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034, huku Mpango wa Taifa wa Nishati ukilenga kufikia asilimia 75 ifikapo mwaka 2030.
Katika hafla hiyo, Dkt.Mataragio amesisitiza umuhimu wa kutumia mifumo ya kifedha ikiwemo dhamana za mikopo, ufadhili mseto na mikopo ya ndani ili kupunguza vihatarishi vya uwekezaji na kuhakikisha miradi ya nishati jadidifu pamoja na nishati safi ya kupikia inaendelea kuwa endelevu.
Aidha ametoa wito kwa Jumuiya ya wadau wa Nishati Jadidifu Tanzania (TAREA) kuendelea kuimarisha nafasi yake katika kuendeleza sekta hiyo, akihimiza wadau kutumia kongamano hilo kujenga ushirikiano, kubuni suluhisho na kuandaa miradi yenye tija kwa taifa.