Featured • Kitaifa

JKT YATANGAZA NAFASI ZA KUJITOLEA KWA VIJANA  KUJIUNGA NA MAFUNZO YA JKT KWA MWAKA 2026/27

Written by Alex Sonna

Mkuu wa Tawi la Utawala Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Brigedia Jenerali Hassan Mabena,akizungumza na Waandishi wa Habari  leo Novemba 12,2026 Makao Makuu ya JKT Chamwino Mkoani Dodoma kwa niaba ya MKUU wa JKT.

Na.Gideon Greogry-CHAMWINO

JESHI la Kujenga Taifa JKT limetangaza nafasi za kujitolea kujiunga na mafunzo ya JKT kwa mwaka 2026/27 kwa vijana wote kutoka Tanzania Bara na Zanzibar wenye sifa za kujiunga na Jeshi  hilo  huku watakaopata nafasi hizo wakitakiwa  kuripoti katika kambi za JKT kuanzia Disemba 10 hadi Disemba, 15,2026.

Akizungumza leo Novemba 12,2026 na Waandishi wa Habari Makao Makuu ya JKT Chamwino Mkoani Dodoma kwa niaba ya MKUU wa JKT,Mkuu wa Tawi la Utawala JKT Brigedia Jenerali Hassan Mabena amesema vijana wenye sifa zinazohitajika wanapaswa kuwasilisha maombi yao kupitia Ofisi za Wakuu wa Mikoa na Wilaya wanakotoka, huku usaili kwa waombaji ukitarajiwa kuanza Novemba 16, 2026, katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Brigedia Jenerali Mabena amesema nafasi hizo zinawahusu wahitimu wa Shahada ya Sayansi ya Mitandao ya Kompyuta na Usalama wa Taarifa (Bachelor of Science in Computer Networks and Information Security), pamoja na walimu wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo (VET) wenye utaalamu katika fani mbalimbali.

Miongoni mwa fani zinazohitajika ni uchomeleaji, ufundi magari, umeme wa magari, ufundi bomba, ufundi rangi, uashi, teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA), ubunifu wa mavazi, ukarani, useremala, ushonaji pamoja na ufundi wa friji na viyoyozi.

Kwa mujibu wa Brigedia Jenerali Mabena, vijana watakaofaulu usaili huo na kuchaguliwa kujiunga na mafunzo watatakiwa kuripoti katika makambi ya JKT kuanzia Desemba 10 hadi 15, mwaka huu.

Hata hivyo, JKT limeweka wazi kuwa mafunzo ya kujitolea si njia ya kupata ajira serikalini au katika taasisi nyingine, likisisitiza kuwa halitoi ajira wala halihusiki kuwatafutia vijana ajira katika asasi, vyombo vya ulinzi na usalama, mashirika ya serikali au yasiyo ya kiserikali.

Badala yake, mafunzo hayo yanalenga kuwajengea vijana nidhamu, uzalendo na ujuzi mbalimbali utakaowawezesha kujitegemea na kujiajiri baada ya kumaliza mikataba yao ya kulitumikia jeshi hilo.

Wakati huohuo, Brigedia Jenerali Mabena amewaonya vijana, wazazi na wananchi kwa ujumla kujihadhari na watu wanaoweza kujitokeza wakidai kuwa wanauza nafasi za kujiunga na JKT kwa kujitolea.

Amesisitiza kuwa nafasi hizo haziuziwi na hakuna malipo yoyote yanayotakiwa kufanywa ili kupata nafasi, huku akiwataka wananchi kutokubali kushawishiwa na matapeli wanaotumia fursa ya matangazo ya kujiunga na jeshi hilo kujipatia fedha kwa njia zisizo halali.

Aidha, wananchi wametakiwa kutoa taarifa kwa vyombo vya dola wanapokutana na watu wanaodai kuwa na uwezo wa kuwapatia vijana nafasi za JKT kwa malipo, ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya wanaojihusisha na vitendo hivyo.

JKT limewahimiza vijana wenye sifa zinazohitajika kutumia fursa hiyo kwa kufuata taratibu rasmi zilizotolewa na kujitokeza kuomba nafasi za kushiriki mafunzo ya kujitolea kwa mwaka 2026/2027.

“Sifa za muombaji na maelekezo ya vifaa wanavyotakiwa kwenda navyo yanapatikana katika Tovuti ya JKT ambayo ni www.ikt.mil.tz ,”amesema.

About the author

Alex Sonna