
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, akizungumza wakati wa kupokea Uenyekiti wa Baraza la Mawaziri la Mamlaka ya Ziwa Tanganyika (LTA), katika Mkutano wa 14 wa Baraza hilo uliofanyika jijini Dar es Salaam, Oktoba 30, 2026.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni akiwa katika Mkutano wa 14 wa Baraza la Mawaziri la Mamlaka ya Ziwa Tanganyika uliofanyika jijini Dar es Salaam, Oktoba 30, 2026, ambapo Tanzania imepokea Uenyekiti wa Baraza hilo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni (wa pili kulia), akiwa na viongozi wengine wakati wa kupokea Uenyekiti wa Baraza la Mawaziri la Mamlaka ya Ziwa Tanganyika (LTA), katika Mkutano wa 14 wa Baraza hilo uliofanyika jijini Dar es Salaam, Oktoba 30, 2026.
PICHA NA OFISI YA MAKAMU WA RAIS
NA; MWANDISHI WETU-DARA ES SALAAM
Tanzania imepokea rasmi jukumu la Uenyekiti wa Baraza la Mawaziri la Mamlaka ya Ziwa Tanganyika (LTA), ikiwa na dhamira ya kuimarisha ushirikiano wa kikanda, usimamizi endelevu wa rasilimali za ziwa na kulinda mazingira kwa manufaa ya wananchi wa nchi wanachama.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, amepokea jukumu hilo katika Mkutano wa 14 wa Baraza la Mawaziri la Mamlaka ya Ziwa Tanganyika uliofanyika jijini Dar es Salaam, Oktoba 30, 2026.
Akizungumza wakati wa kukubali jukumu hilo kutoka Zambia, Mhe. Masauni amesema Tanzania inalichukulia jukumu la uenyekiti kama dhamana kubwa inayohitaji mshikamano, uwajibikaji na hatua za pamoja za nchi zote nne zinazopakana na Ziwa Tanganyika ambazo ni Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Tanzania na Zambia.
Amesema Ziwa Tanganyika ni urithi wa pamoja wenye umuhimu mkubwa kiikolojia, kiuchumi na kijamii, likiwa chanzo muhimu cha chakula, ajira, kipato na hifadhi ya bioanuai yenye umuhimu wa kimataifa.
“Tanzania itatumia kipindi chake cha uenyekiti kuimarisha ushirikiano wa kikanda na uratibu wa kitaasisi, kuendeleza usimamizi jumuishi wa ziwa na bonde lake, pamoja na kuongeza juhudi za kukabiliana na uchafuzi wa mazingira, uvuvi usio endelevu, uharibifu wa ardhi na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Aidha, amesema Serikali itaweka mkazo katika kuimarisha upatikanaji wa fedha endelevu kwa ajili ya utekelezaji wa programu na miradi ya Mamlaka ya Ziwa Tanganyika, huku ikihimiza nchi wanachama kutekeleza wajibu wao wa michango na washirika wa maendeleo kuendelea kutoa msaada wa kifedha, kitaalamu na kiteknolojia.
“Tanzania itaunga mkono mipango inayokuza uvuvi endelevu, kuboresha huduma za usafi wa mazingira, kuzuia uchafuzi wa maji na kuongeza ushiriki wa wanawake, vijana na jamii zinazotegemea rasilimali za ziwa katika shughuli za maendeleo.”
Amesema Tanzania itaendelea kushirikiana kwa karibu na nchi zote wanachama pamoja na wadau wa maendeleo katika kutekeleza Mkataba wa Usimamizi Endelevu wa Ziwa Tanganyika, akibainisha kuwa hakuna nchi inayoweza kulinda ziwa hilo kwa mafanikio kwa kuchukua hatua peke yake.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Uchumi wa Buluu na Mazingira nchini Zambia, Dkt. Douty Chibamba amesema mafanikio ya Mamlaka ya Ziwa Tanganyika hayatapimwa kwa idadi ya maazimio tunayopitisha pekee, bali kwa matokeo halisi yanayopatikana katika kulinda ziwa, kuboresha maisha ya wananchi na kuimarisha maendeleo ya kikanda.
Vilevile, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha utekelezaji wa maazimio ya Baraza la Mawaziri kwa kuhakikisha kunakuwa na mgawanyo wa majukumu ulio wazi, rasilimali za kutosha na mifumo madhubuti ya kufuatilia na kutathmini maendeleo ya programu na miradi.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Ziwa Tanganyika, Dkt. Emma Liwenga Ameeleza kuwa uhifadhi wa mazingira unapaswa kwenda sambamba na kuboresha maisha ya wananchi na kuimarisha uchumi wa nchi zinazozunguka ziwa hilo.
Amesema kulinda Ziwa Tanganyika si jukumu la kimazingira pekee, bali pia ni kipaumbele cha maendeleo, wajibu wa kikanda na uwekezaji muhimu kwa maisha na mustakabali wa wananchi.