Featured • Kitaifa

UMALITA WARIDHISHWA MIKAKATI YA SERIKALI KUWAENDELEZA KIUCHUMI

Written by Alex Sonna

Na WMJJWM Dodoma

Umoja wa Mama na Baba Lishe Tanzania (UMALITA), wameridhishwa na mikakati ya Serikali ya kuwatambua na kuwaendeleza kiuchumi ili watoke kqenye biashara ya kujikimu na kuwa na malengo makubwa.

Hayo yamebainika katika ziara ya umoja huo waliyoifanya katika Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Oktoba 29, 2026 Mtumba jijini Dodoma.

Akizungumza katika kikao na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Eliakim Maswi, Mwenyekiti wa UMALITA Havijawa Omary amesema Serikali ya Awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan imefanya kazi kubwa na wao kama sehemu ya wanufaika wamefurahi kujionea miundombinu bora iliyowekwa ili kuwahudumia wananchi.

Amesema wako tayari kumsaidia Rais kuhakikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inatekelezeka hasa kuhakikisha ustawi na uchumi wa watu.

“Ustawi na uchumi wa watu unaimarika iwapo pia wanakuwa na afya njema. Tuko radhi kutoa shilongi elfu 2 kila siku ili kujiunga na mfuko wa Bima ya Afya kwa wote kwa sababu kuna baadhi yetu wanakopa hadi mikopo ya kausha damu ili kupata matibabu”

Naye mmiliki wa Migahawa maarufu ya Kitambaa Cheupe, Jessica Kikumbi amepata nafasi ya kushiriki ziara hiyo ambapo amewasihi Baba na Mama Lishe kuitumia vizuri fursa ya kutambuliwa na Serikali kujiimarisha Kiuchumi.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Eliakim Maswi amewaeleza UMALITA kuwa, Serikali inaandaa mikakati ya kuwatambua Baba na Mama lishe wote nchini iwe rahisi kuwaratibu na kutumia fursa zilizopo kwa ufanisi.

Maswi amebainisha kwamba Serikali inatambua changamoto za mama na baba lishe nchini za kutokuwa na uhakika wa maeneo ya biashara, masoko, miundombinu safi, mitaji, afya, lishe na usalama. Hivyo amewahakikishia kundi hilo litaratibiwa vizuri na matokeo yake litafanya mambo makubwa baada ya kutambuliwa na kujisajiliwa.

“Mnatoa huduma ya chakula na mnatengeneza Ajira, mnaunganisha masoko ya wakulima, wafugaji, wavuvi na wafanyabiashara wa bidhaa mbalimbali” amesema Maswi.

About the author

Alex Sonna