Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema kujenga ustahimilivu dhidi ya maafa ni wajibu wa pamoja unaohitaji ushiriki wa serikali, sekta binafsi na jamii, akisisitiza umuhimu wa maandalizi kuanzia katika ngazi ya kaya.
Dkt. Mwigulu amesema hayo leo, Oktoba 13, 2026, wakati akitoa tamko la kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kupunguza Hatari ya Maafa katika Uwanja wa Nelson Mandela, Sumbawanga, mkoani Rukwa.
Amesema serikali itaendelea kuimarisha mifumo ya kuzuia na kupunguza athari za maafa katika ngazi ya taifa na jamii, kuboresha utoaji wa taarifa na kuongeza uhamasishaji wa umma kuhusu hatua za tahadhari na maandalizi.
Waziri Mkuu amesisitiza kuwa familia ndiyo msingi wa jamii, hivyo usalama na ustahimilivu wa kaya ni muhimu katika kuijengea jamii uwezo wa kujiandaa, kukabiliana na maafa na kurejesha hali ya kawaida baada ya kutokea.
Aidha, amehimiza mamlaka za serikali za mitaa, taasisi za utafiti, mashirika yasiyo ya kiserikali, vyombo vya habari, taasisi za dini na viongozi wa kimila kushiriki katika kuimarisha maandalizi na ustahimilivu wa jamii dhidi ya maafa.
Akizungumzia maandalizi ya msimu wa mvua za vuli wa Oktoba hadi Desemba, amewataka wananchi kuzingatia tahadhari zilizotolewa na kujiandaa mapema ili kupunguza hatari na athari za maafa.