Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), akizungumza katika kikao kilichojadili hali na mwelekeo wa Africa Credit Rating Agency (AfCRA), mpango wa Umoja wa Afrika (AU) unaolenga kuanzisha taasisi ya ukadiriaji wa mikopo inayomilikiwa na kuendeshwa kwa misingi ya sekta binafsi, kilichofanyika jijini New York, Marekani.

Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), (wa pili kushoto), wakiwa katika picha ya pamoja na ujumbe wa Tanzania, mara baada ya kukamilika kwa kikao kilichojadili hali na mwelekeo wa Africa Credit Rating Agency (AfCRA), mpango wa Umoja wa Afrika (AU) unaolenga kuanzisha taasisi ya ukadiriaji wa mikopo inayomilikiwa na kuendeshwa kwa misingi ya sekta binafsi, kilichofanyika jijini New York, Marekani.

Picha za matukio mbalimbali wakati Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), aliposhiriki katika kikao kilichojadili hali na mwelekeo wa Africa Credit Rating Agency (AfCRA), mpango wa Umoja wa Afrika (AU) unaolenga kuanzisha taasisi ya ukadiriaji wa mikopo inayomilikiwa na kuendeshwa kwa misingi ya sekta binafsi, kilichofanyika jijini New York, Marekani.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, New York, Marekani)
Na. Scola Malinga, WF, New York, Marekani.
Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb.), ameshiriki katika kikao kilichojadili hali na mwelekeo wa Africa Credit Rating Agency (AfCRA), mpango wa Umoja wa Afrika (AU) unaolenga kuanzisha taasisi ya ukadiriaji wa mikopo inayomilikiwa na kuendeshwa kwa misingi ya sekta binafsi. AfCRA imeundwa kama taasisi ya kibiashara inayojigharamia na kujitegemea kifedha, tofauti na taasisi za kawaida za AU, huku African Peer Review Mechanism (APRM) ikipewa jukumu la kuongoza mchakato wa uanzishwaji wake.
Kikao kimeelezwa kuwa AfCRA inapaswa kueleweka kama taasisi ya kibiashara yenye uungwaji mkono wa kisiasa kutoka AU, huku APRM ikiwa mdhamini na kiongozi wa utekelezaji katika hatua ya uanzishwaji. Uzinduzi rasmi wa AfCRA umepangwa kufanyika tarehe 7 Oktoba 2026, jijini Port Louis, Mauritius.
Katika kuhakikisha taasisi hiyo inajenga uaminifu katika soko la fedha, msisitizo umewekwa kwenye umuhimu wa kuwepo kwa uhuru wa kitaalamu, uwazi wa mifumo ya uendeshaji na kuhakikisha kuwa maamuzi ya ukadiriaji hayaathiriwi na masuala ya kisiasa.
Aidha, kikao kimeweka msisitizo wa kuendelea kuunga mkono wazo la kuwa na taasisi ya ukadiriaji wa mikopo inayomilikiwa na Waafrika, huku uaminifu, uwazi, uhuru wa kitaasisi na uendelevu wa kifedha vikitiliwa mkazo. Sambamba na hilo, imependekezwa kuwa ushiriki wa nchi wanachama katika mpango wa AfCRA uendelee kuwa wa hiari, huku nafasi ya Serikali ikiendelea kulenga kuhakikisha kuwa taasisi hiyo inajengwa kwa misingi ya uwajibikaji, weledi na uaminifu katika ukadiriaji wa mikopo.
Kikao hicho kimefanyika pembezoni mwa Mkutano wa Ngazi ya Juu wa Jukwaa la Kimataifa la Fedha za Mabadiliko ya Tabianchi (Private Climate Finance Community). Mkutano huo ulioratibiwa na Baraza la Uchumi la Dunia (WEF) kama sehemu ya Mikutano ya Athari za Maendeleo Endelevu 2026 (SDIM26), ulifanyika katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa (UN) jijini New York, Marekani.