Featured Kitaifa

LUSWETULA: SERIKALI YAWEKA MKAZO PPP KUGHARIMIA SEKTA YA AFYA

Written by Alex Sonna


Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb), akieleza umuhimu wa Ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi (PPP) kama moja ya njia muhimu za kuongeza upatikanaji wa fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo, wakati wa mdahalo kuhusu vyanzo vya fedha kwa ajili ya kuendeleza Sekta ya Afya, uliofanyika Nairobi, Kenya.

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb), akiteta jambo na Bw. Deus Bazira kutoka Chuo Kikuu cha Georgetown, baada ya kumalizika kwa mdahalo kuhusu vyanzo vya fedha kwa ajili ya kuendeleza Sekta ya Afya, wakati wa Jukwaa la Mazungumzo ya Ngazi za Juu la Mawaziri wa Fedha, Nairobi, Kenya.

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb), akiwa katika mdahalo kuhusu vyanzo vya fedha kwa ajili ya kuendeleza Sekta ya Afya, uliofanyika Nairobi, Kenya.

Wajumbe kutoka Tanzania walioambatana na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb), Nairobi, Kenya, wakifuatilia mdahalo kuhusu vyanzo vya fedha kuwezesha Sekta ya Afya, wakati wa Jukwaa la Mazungumzo ya Ngazi za Juu la Mawaziri wa Fedha wa Afrika.

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb), akiagana na Mratibu Msaidizi wa Masuala ya Fedha wa Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania, Bw. Omar Kebbeh, baada ya kumalizika kwa mdahalo kuhusu vyanzo vya fedha kuwezesha Sekta ya Afya, wakati wa Jukwaa la Mazungumzo ya Ngazi za Juu la Mawaziri wa Fedha wa Afrika, Nairobi, Kenya.

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb), akiwa katika picha ya pamoja na Mratibu Msaidizi wa Masuala ya Fedha wa Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania, Bw. Omar Kebbeh (kulia), baada ya kumalizika kwa mdahalo kuhusu vyanzo vya fedha kuwezesha Sekta ya Afya, wakati wa Jukwaa la Mazungumzo ya Ngazi za Juu la Mawaziri wa Fedha, lililofanyika Nairobi, Kenya. Wengine ni wajumbe kutoka Wizara ya Fedha na Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania.

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb), akizungumza na wajumbe wa Jukwaa la Mazungumzo ya Ngazi za Juu la Mawaziri wa Fedha, Nairobi, Kenya, lililoandaliwa na Serikali ya Marekani.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha, Naironi-Kenya)

Na Peter Haule, WF, Nairobi, Kenya

Serikali ya Tanzania imeeleza kuwa inaendelea kuimarisha vyanzo vyake vya ndani vya fedha pamoja na matumizi ya mfumo wa Ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi (PPP) katika kugharamia miradi ya maendeleo, ikisisitiza kuwa mikopo ya Serikali itaelekezwa katika miradi yenye manufaa ya muda mrefu kiuchumi na kijamii.

Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb), wakati wa mdahalo ulioongozwa na Mtaalamu wa Idara ya Hazina ya Marekani, Bw. Eric Meyer, kuhusu vyanzo vya fedha kwa ajili ya kuendeleza Sekta ya Afya, wakati wa Jukwaa la Mazungumzo ya Ngazi za Juu la Mawaziri wa Fedha, lililofanyika Nairobi, Kenya.

Mhe. Luswetula, aliyemwakilisha Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar katika mkutano huo, alisisitiza umuhimu wa Ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi (PPP) kuwa moja ya njia muhimu za kuongeza upatikanaji wa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

“Tanzania iko tayari kushirikiana na sekta binafsi kupitia mikataba ya muda mrefu katika utekelezaji wa miradi mbalimbali. Tunakaribisha kampuni na wawekezaji kushirikiana na Serikali katika uwekezaji wenye tija,” alisema Mhe. Luswetula.

Alisema Sera ya Serikali inalenga kukuza uwekezaji, kuongeza shughuli za kiuchumi na kuhakikisha sekta binafsi inapata nafasi kubwa zaidi katika kuchochea maendeleo ya Taifa.

Vilevile, Mhe. Luswetula alisema Serikali inatumia ushuru wa bidhaa (excise duty) kama moja ya njia za kulinda afya za wananchi dhidi ya athari hasi zinazoweza kusababishwa na baadhi ya bidhaa, huku mapato yatokanayo na kodi hiyo yakisaidia kugharamia huduma na miundombinu ya afya.

Alisema ukusanyaji wa mapato kupitia kodi hizo ni sehemu ya juhudi za Serikali kuongeza uwezo wa ndani wa kugharamia huduma za kijamii na kupanua wigo wa mapato ya Taifa.

Akizungumzia suala la mikopo, Mhe. Luswetula alisema Serikali haitumii mikopo bila kuzingatia uwezo wa miradi husika kuzalisha manufaa ya muda mrefu na kuchangia katika ulipaji wa madeni.

Alisema kipaumbele kinatolewa kwa miradi ya kimkakati, ikiwemo miundombinu ya msingi na uwekezaji mwingine wa mitaji wenye manufaa ya muda mrefu kwa uchumi na jamii.

“Hatutaki kukopa kwa sababu tu tunataka kupata fedha. Tunakopa pale ambapo uwekezaji una manufaa ya muda mrefu na tuna uhakika wa namna ya kurejesha deni,” alisema Mhe. Luswetula.

Alisema utaratibu huo unalenga kuhakikisha kuwa mikopo ya Serikali inatumika kwa nidhamu na kuelekezwa katika miradi inayoweza kutoa matokeo yanayostahili gharama ya fedha hizo.

Mhe. Luswetula alisema Tanzania inaendelea kutoka katika mfumo wa kutegemea zaidi fedha za wafadhili na kuelekea katika mfumo unaochanganya rasilimali za ndani, ufadhili wa pamoja na uwekezaji wa sekta binafsi.

About the author

Alex Sonna