Dodoma
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) umeendelea kuboresha miundombinu ya barabara na madaraja katika jiji la Dodoma hatua inayolenga kuwa na miundombinu imara na salama kwa wananchi itakayoweza kihimili mabadiliko ya tabia nchi ikiwemo mvua za el-nino.
Hayo yamesemwa na Meneja wa TARURA wilaya ya Dodoma Mhandisi Emmanuel Mfinanga wakati wa ukaguzi wa miradi mbalimbali inayotekelezwa na Wakala huo katika maeneo mbalimbali ya Jiji hilo.
Mhandisi Mfinanga amesema katika eneo la Ntyuka wamejenga madaraja matatu ya mawe yenye urefu wa mita 14 kwa gharama ya shilingi milioni 398 jambo ambalo limesaidia kupunguza gharama za ujenzi kwani wangetumia zege wangejenga angalau daraja moja tu.
Amesema uwepo wa madaraja hayo umeendelea kurahisisha usafiri na usafirishaji kwa wananchi hususan wanaoishi maeneo ya nyuma ya reli ya SGR ambao sasa wanaweza kufika mjini kwa urahisi zaidi.
Katika hatua nyingine, Mhandisi Mfinanga amesema wameendelea kuboresha barabara ya Ilazo–Mbuyuni ambapo awali kulikuwa na ujenzi wa kilomita 1 ya barabara bila kuwepo mitaro ya maji ya mvua lakini sasa wamepata fedha shilingi milioni 759 kwa ajili ya ujenzi wa barabara mita 250 kwa kiwango cha lami pamoja na ujenzi wa mitaro kilomita 1.5.
Amesema hatua hiyo imelenga kuimarisha barabara na kuhakikisha inakuwa salama na inapitika wakati wote hususan katika kipindi cha mvua ambapo maji yanaweza kusababisha uharibifu wa barabara endapo mifumo ya kuondoa maji haitakuwa imara.
Akizungumzia barabara ya Nala–Viwandani, Mhandisi Mfinanga amesema barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 5.18 imejengwa kwa kiwango cha lami ikiwa na mifereji pamoja na taa za barabarani.
Amesema barabara hiyo imekuwa na umuhimu mkubwa katika kuchochea shughuli za kiuchumi kwa wananchi wa kata ya Nala kwa kuwa inaunganisha maeneo ya viwanda ambapo amewaomba wananchi wa Nala washirikiane kutunza miundombinu hususan taa za barabarani ili iweze kudumu na kuendelea kuwanufaisha wananchi hao.
Aidha, Mhandisi Mfinanga amesema TARURA inatarajia kuanza kutekeleza mradi wa kupunguza msongamano wa magari katikati ya Jiji la Dodoma (DIST) ambao utahusisha maeneo mbalimbali ndani ya jiji.
Amesema mradi huo unatarajiwa kuwa sehemu ya hatua za kukabiliana na changamoto ya foleni inayoweza kujitokeza kutokana na kasi kubwa ya ukuaji wa Jiji la Dodoma na ongezeko la shughuli za kiuchumi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi wa Jiji la Dodoma wameeleza kuridhishwa na maboresho ya miundombinu ya barabara na madaraja yanayotekelezwa na TARURA wakisema miradi hiyo imeanza kuleta mabadiliko chanya katika usafiri, shughuli za kiuchumi na kuongeza kasi ya maendeleo katika maeneo yao.
Kwa ujumla miradi hiyo inaonesha jitihada za TARURA katika kuimarisha mtandao wa barabara na madaraja, kurahisisha shughuli za kijamii na kiuchumi sambamba na kuhakikisha miundombinu ya jiji la Dodoma inaendana na kasi ya ukuaji wake.
