Featured • Kitaifa

CCM YARIDHISHWA NA UJENZI WA SKULI YA SEKONDARI KAMA

Written by Alex Sonna

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Ndugu Abdi Mahamoud Abdi, amesema CCM imeridhishwa na hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa Skuli ya Sekondari Kama, akieleza kuwa mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa vitendo.

Ndugu Abdi ameyasema hayo leo, Oktoba 3, 2026, wakati akiendelea na ziara yake ya kukagua uhai wa Chama hicho pamoja na kusikiliza changamoto za wananchi, ambapo ametembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Skuli ya Sekondari Kama.

Amesema ujenzi wa miundombinu ya kisasa ya elimu ni miongoni mwa jitihada za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kutekeleza Ilani ya CCM, hatua ambayo inalenga kurahisisha upatikanaji wa huduma za elimu na kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi.

Ndugu Abdi ameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwa kuendelea kutekeleza Ilani ya CCM kwa vitendo kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo sekta ya elimu.

Aidha, amesema CCM itaendelea kufuatilia na kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi inayotekelezwa na Serikali, huku akiwataka walimu, wananchi na wasimamizi wa mradi huo kuhakikisha ujenzi unakamilika kwa wakati ili skuli hiyo ianze kutoa huduma kwa wananchi.

Kwa upande wake, Mshauri wa Kazi wa mradi huo, Ndugu Abeli Beni, amesema ujenzi wa Skuli ya Sekondari Kama umefikia asilimia 80 na kwamba mradi huo unakadiriwa kugharimu Sh bilioni 3 hadi kukamilika.

Amesema mradi huo unatarajiwa kukamilika mwezi Novemba mwaka huu.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Magharibi A, Ndg. Laila Burhan Ngozi, amesema mradi huo unaendelea vizuri na kwamba ameridhishwa na hatua iliyofikiwa katika ujenzi wake.

Amesema kukamilika kwa skuli hiyo kutasaidia kupunguza changamoto ya msongamano wa wanafunzi madarasani na hivyo kuboresha mazingira ya utoaji na upatikanaji wa elimu katika eneo hilo.

About the author

Alex Sonna