
Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Prof. William Amos Pallangyo, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Septemba 07, 2026, katika ukumbi wa Idara ya Habari – MAELEZO, kuhusu utekelezaji wa Taasisi hiyo katika kipindi cha mwaka wa fedha 2025/26 na mwelekeo wa 2026/27.
Na.Alex Sonna,Mzalendo blog-DODOMA
WAKATI changamoto ya ajira ikiendelea kuwa miongoni mwa masuala yanayowakabili vijana wanaohitimu elimu ya juu, Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) imeweka mkazo katika kuwajengea wanafunzi uwezo wa kutumia maarifa wanayopata chuoni kubuni suluhisho, kuanzisha biashara na kujiajiri, badala ya kutegemea ajira pekee.
Hatua hiyo imebainishwa leo, Septemba 7, 2026, jijini Dodoma na Afisa Mtendaji Mkuu wa TIA, Prof. William Pallangyo, wakati akizungumza na vyombo vya habari kuhusu utekelezaji wa shughuli za taasisi hiyo katika mwaka wa fedha 2025/26 na mwelekeo wa mwaka wa fedha 2026/27.
Prof. Pallangyo amesema kupitia Kitengo cha Ukuzaji na Uendelezaji wa Wanafunzi Kitaaluma na Kitaalamu, zaidi ya wanafunzi 5,000 wamefikiwa kupitia warsha zinazohusu ujasiriamali, ubunifu, ajira na fursa za kimataifa.
Amesema zaidi ya wanafunzi 500 wamepata mafunzo mahsusi ya ujasiriamali, huku takribani wanafunzi 100 wakisaidiwa kuanzisha biashara ndogo ndogo, hatua inayolenga kuwajengea uwezo wa kujitegemea na kuongeza mchango wao katika uchumi.
“Pamoja na kuwafikia wanafunzi zaidi ya 5,000 kupitia warsha zinazohusu ujasiriamali, ubunifu, ajira na fursa za kimataifa, zaidi ya wanafunzi 500 wamepata mafunzo mahsusi ya ujasiriamali, huku takribani 100 wakisaidiwa kuanzisha biashara ndogo ndogo,” amesema Prof. Pallangyo.
Amesema matokeo ya mpango huo yanaonekana kupitia wanafunzi walioweza kubadilisha mawazo yao kuwa bidhaa na mifumo inayolenga kutatua changamoto za jamii, akitolea mfano SmartGlove, teknolojia inayolenga kuvunja kikwazo cha mawasiliano kwa watu wenye changamoto za usikivu.
“Teknolojia hiyo inalenga kutafsiri lugha ya alama kuwa maneno yanayosikika, kwa lengo la kusaidia watu wenye changamoto za usikivu katika mawasiliano,” amesema.
Prof. Pallangyo amesema wazo la SmartGlove lilibuniwa na mwanafunzi Damian Msonge baada ya kushuhudia kijana mwenye ulemavu wa kusikia akifikishwa hospitalini akiwa katika hali ya dharura, lakini akakumbana na changamoto ya kueleza hali yake kwa lugha ya alama kutokana na kutokuwepo kwa mkalimani kwa wakati huo.
Kwa mujibu wa Prof. Pallangyo, mfano huo unaonyesha namna TIA inavyolenga kuwajengea wanafunzi uwezo wa kutambua changamoto zinazowakabili wananchi na kutumia maarifa pamoja na teknolojia kuzitafutia suluhisho, badala ya kuishia katika kupata vyeti pekee.
Akizungumzia mwelekeo wa mwaka wa fedha 2026/27 na miaka inayofuata, Prof. Pallangyo amesema TIA itaendelea kutekeleza mipango yake kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Mpango Mkakati mpya wa TIA wa mwaka 2026/27 hadi 2030/31 pamoja na miongozo ya Serikali.
Amesema miongoni mwa vipaumbele vya taasisi hiyo ni kuongeza ubora wa elimu kwa kuimarisha uwezo wa wahadhiri na watumishi zaidi ya 400, kuboresha huduma za maktaba na intaneti, kuendeleza utafiti na ushauri wa kitaalamu pamoja na kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika huduma za wanafunzi na usimamizi wa taasisi.
Katika eneo la miundombinu, TIA inalenga kukamilisha miradi ya kimkakati katika kampasi za Kigoma, Mwanza, Zanzibar na Singida. Aidha, taasisi hiyo inapanga kujenga jengo jipya la taaluma katika eneo la Gezaulole, Kigamboni, kwa lengo la kuongeza uwezo wa Kampasi ya Dar es Salaam na kupunguza msongamano katika Makao Makuu.
Vilevile, TIA inalenga kupata eneo kwa ajili ya Kampasi mpya ya Tanga na kukamilisha taratibu za fidia ya eneo la Zanzibar, huku ikiandaa mpango wa miaka 25 wa 2026 hadi 2050 utakaokwenda sambamba na Dira ya Taifa 2050.
Mpango huo wa muda mrefu unatarajiwa kuweka mwelekeo wa TIA katika maeneo ya elimu, utafiti, ubunifu, TEHAMA, miundombinu na ushirikiano wa kimataifa, hatua inayolenga kuiwezesha taasisi hiyo kwenda sambamba na mahitaji ya uchumi wa kisasa na soko la ajira.
Kwa ujumla, mwelekeo huo unaashiria mabadiliko ya TIA kutoka taasisi iliyojikita katika utoaji wa elimu ya uhasibu pekee kwenda taasisi inayolenga kuzalisha wataalamu, wabunifu, watafiti na wajasiriamali wenye uwezo wa kuchangia moja kwa moja katika uchumi na maendeleo ya Taifa.
Kwa mtazamo huo, mafanikio ya TIA hayatapimwa kwa idadi ya wanafunzi wanaohitimu pekee, bali pia kwa uwezo wa wahitimu kutumia elimu na maarifa waliyopata kutengeneza ajira, kuanzisha biashara na kubuni suluhisho zinazoweza kuboresha maisha ya wananchi.