Na, Mwandishi Wetu -Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuzindua majengo ya Ofisi za Wizara, Taasisi za Serikali pamoja na barabara za lami zenye urefu wa kilomita 57.1 katika Mji wa Serikali Mtumba,Jijini Dodoma.
Uzinduzi huo unatarajiwa kufanyika jumanne Septemba nane mwaka huu katika Uwanja wa Mashujaa uliopo ndani ya Mji wa Serikali Mtumba.
Hayo yamebainishwa Jijini Dodoma leo (06 Septemba, 2026) na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Mhe.Profesa Palamagamba Kabudi, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya hafla hiyo.
Alisema uzinduzi huo utahusisha maeneo matatu makuu ambayo ni majengo ya Ofisi za Wizara 26, Taasisi 11 za Serikali na barabara za lami zenye urefu wa kilomita 57.1.
Profesa Kabudi alisema kukamilika kwa majengo hayo, kutawezesha watumishi 18,510 kutumia ofisi za Mji wa Serikali, Mtumba.
“Ujenzi wa Mji wa Serikali Mtumba ulianza kutekelezwa kwa awamu, ambapo awamu ya kwanza ilihusisha ujenzi wa majengo 23 ya Ofisi za muda.ujenzi wa majengo hayo ulianza Novemba 28 mwaka 2018 na kukamilika Machi 22 mwaka 2019, hatua iliyowezesha baadhi ya watumishi wa Wizara na taasisi kuanza kuhamia.
Aliongeza kuwa :” Awamu ya pili ya ujenzi ilianza Oktoba, 2021, ikiwa inalenga kujenga majengo ya kudumu kwa ajili ya watumishi wote wa Wizara na Taasisi zilizopangwa kuhamia Mtumba.Pia ilihusisha ujenzi wa miundombinu na huduma mbalimbali za kijamii, ikiwemo barabara za lami.
Profesa Kabudi alisema mbali na barabara hizo, miundombinu ya kudumu ya mawasiliano pamoja na Uwanja wa Mashujaa imekamilika na itakuwa sehemu ya miundombinu itakayotumika katika shughuli za Serikali.
Hata hivyo, alisema baadhi ya miradi bado iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji, ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya umeme inayopita chini ya ardhi yenye urefu wa kilomita 42.
“Kazi ya ujenzi wa miundombinu ya maji safi na uondoshaji wa maji taka, TEHAMA, ufungaji wa mifumo ya usalama ya CCTV Camera, ujenzi wa kituo cha zimamoto pamoja na utekelezaji wa mpango wa upandaji miti na ustawishaji wa Mji wa Serikali nazo zinafanyika, “alisema.
Alisema Rais Dkt.Samia ameendelea kuweka msisitizo katika kuboresha mazingira hayo, ikiwa ni pamoja na kutoa fedha kwa ajili ya ununuzi wa samani za Wizara na taasisi 26 zinazohamia katika majengo hayo.
Profesa Kabudi alisema hatua hizo zinaendelea kuifanya Mji wa Serikali Mtumba kuwa miongoni mwa alama muhimu za utekelezaji wa dhana ya Dodoma kuwa kitovu cha shughuli za Serikali.
Alisema uwekezaji huo pia unatarajiwa kuongeza fursa za kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa Dodoma na Tanzania kwa ujumla.