Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), akichangia jambo wakati wa kikao cha Mfuko wa Ushirikiano wa Maendeleo ya Miundombinu (MCDF) kilichowashirikisha Mawaziri wa Fedha ambao ni Magavana wa Benki ya Maendeleo ya Miundombinu ya Asia (AIIB), kilichofanyika kando ya Mkutano wa 11 wa Mwaka wa Magavana wa Benki hiyo, jijini Doha, nchini Qatar.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Doha nchini Qatar)
Na Benny Mwaipaja, Doha, Qatar
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), amesema kuwa Tanzania inahimiza umuhimu wa ushirikiano wake na Mfuko wa Ushirikiano wa Maendeleo ya Miundombinu (MCDF) katika kuimarisha miradi ya kimkakati na kuchochea maendeleo endelevu nchini.
Mhe. Balozi amesema hayo wakati akihutubia katika kikao cha Mfuko huo kilichowashirikisha Mawaziri wa Fedha ambao ni Magavana wa Benki ya Maendeleo ya Miundombinu ya Asia (AIIB), kilichofanyika kando ya Mkutano wa 11 wa Mwaka wa Magavana wa Benki hiyo, jijini Doha, nchini Qatar.
Alisema kuwa Tanzania inaridhishwa na mchango wa Mfuko huo katika kuandaa miradi yenye ubora na inayoweza kuvutia uwekezaji.
“Tangu kujiunga na MCDF kama mtazamaji mwezi Julai mwaka jana, Tanzania Taasisi ratibu ikiwemo Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), imenufaika na ruzuku ya takriban dola milioni 6.7 za Marekani kwa ajili ya kuandaa miradi mitatu ya kimkakati, ikiwemo miradi ya kikanda katika sekta ya nishati (Mradi wa kuunganisha umeme wa 400KV wa Tanzania na Malawi na Mradi wa kuzalisha na kusambaza umeme wa Bonde la Songwe) na Mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa wa Tanzania na Burundi (Standard Gauge Railway)” alisema Mhe. Balozi Omar
Mhe. Balozi Omar alisema kuwa, ushirikiano huo umekuja wakati mwafaka ambapo Tanzania inatekeleza mpango wake wa nne wa maendeleo wa miaka mitano (2026/2027 hadi 2030/31), unaolenga kukuza mabadiliko ya kiuchumi kupitia uwekezaji katika nishati, usafirishaji, na teknolojia ya kidijitali.
Aliahidi kuwa Tanzania itaendeleza ushirikiano wake na MCDF, Benki ya Uwekezaji ya Miundombinu ya Asia (AIIB), na washirika wengine wa maendeleo na kukaribusha mpango mkakati mpya wa Mfuko huo, wa mwaka 2027-2031, akisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kikanda, ubora wa miradi, na kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.
Kwa upande wake, Rais wa Benki ya Uwekezaji ya Miundombinu ya Asia (AIIB) Bi. Zou Jiayi, amesisitiza umuhimu wa Mfuko wa Ushirikiano wa Maendeleo ya Miundombinu (MCDF) katika kusaidia nchi zinazoendelea kupata miradi ya miundombinu inayoweza kufadhiliwa.
Alibainisha kuwa MCDF si tu mfuko wa uaminifu bali ni mshirika wa kimkakati. Alieleza kuwa MCDF inasaidia kugeuza mahitaji ya uwekezaji kuwa miradi inayoweza kutekelezeka kwa kutoa msaada wa kiufundi na kujenga uwezo.
“Mfuko huu unabadilisha mfumo wake wa biashara ili kujumuisha ufadhili wa daraja na sekta mpya kama nyumba janja na elimu ya kidijitali kwa kuwa kuna mabadiliko katika ufadhili wa maendeleo, ambapo nchi zinazoibukia zinachangia zaidi, jambo linaloonyesha ushirikiano wa Kusini-Kusini” alisema Bi. Jiayi
Ameahidi kuwa AIIB itaendelea kusaidia MCDF katika awamu yake mpya kuanzia mwaka 2027, kwa kuzingatia uwazi na nidhamu katika matumizi ya rasilimali zitakazochangiwa na nchi wanachama pamoja na wadau wengine.



