Na.Alex Sonna,Mzalendo blog-DODOMA
WAKALA wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) umeanza kutumia teknolojia ya kisasa kufanya uchunguzi wa kina wa udongo kabla ya ujenzi wa miradi mikubwa ya miundombinu, hatua inayolenga kuongeza usalama, ubora na uimara wa miradi nchini.
Hatua hiyo inawawezesha wataalamu kupata taarifa za kina kuhusu tabaka za udongo na miamba zilizopo chini ya ardhi, hivyo kusaidia kubaini aina ya msingi na mbinu za ujenzi zinazofaa kulingana na mazingira ya eneo husika.
Hayo yameelezwa leo Septemba 7,2026 jijini Dodoma na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Tafiti na Udhibiti Ubora TARURA, Mhandisi Vincent Lwanda, amesema uchunguzi wa udongo ni miongoni mwa hatua muhimu katika kuhakikisha miundombinu inayojengwa inakuwa salama, imara na yenye uwezo wa kudumu kwa muda mrefu.
Amesema TARURA imekuwa ikifanya tafiti kuhusu udongo pamoja na vifaa mbalimbali vinavyotumika katika ujenzi, huku taarifa zinazopatikana kupitia vipimo hivyo zikitumika kuwawezesha wataalamu kufanya maamuzi sahihi wakati wa kupanga na kutekeleza miradi.
Kwa mujibu wa Mhandisi Lwanda, TARURA imewekeza takribani Sh bilioni mbili katika mtambo maalumu unaotumika kuchimba ardhi na kuchukua sampuli za udongo na miamba kutoka kwenye kina cha chini ya uso wa ardhi kwa ajili ya uchunguzi wa kitaalamu.
“Maabara hizi hazitumiki kwa ajili ya barabara pekee. Wananchi wanaofanya ujenzi wanaweza kuleta vifaa vyao na kupima ubora wake,” amesema Mhandisi Lwanda.
Amesema kwa ajili ya kuimarisha udhibiti wa ubora, TARURA ina maabara kuu pamoja na maabara nyingine 16 katika mikoa mbalimbali nchini ambazo hutumika kupima ubora wa kazi na vifaa vya ujenzi.
Kwa upande wake Mhandisi wa Vifaa wa Kitengo cha Tafiti na Udhibiti Ubora TARURA Makao Makuu, Emmanuel Kilasi, amesema kifaa hicho kinachojulikana kitaalamu kama drilling rig hutumika kuchimba na kutoa sampuli za udongo kwa ajili ya uchunguzi wa hali ya ardhi.
“Taarifa zinazopatikana kupitia sampuli hizo husaidia kubaini uwezo wa udongo kubeba mzigo, jambo ambalo ni muhimu katika kupanga misingi ya miundombinu mikubwa kama madaraja, barabara na majengo.”amesema Mhandisi Kilasi
Amesema mtambo huo una uwezo wa kuchimba hadi kina cha kati ya mita 200 na 300, ambapo sampuli zinazopatikana hupelekwa kufanyiwa vipimo kwa kutumia vifaa maalumu ili kubaini sifa mbalimbali za udongo kabla ya ujenzi kuanza.
Amesisitiza kuwa upatikanaji wa taarifa sahihi kuhusu hali ya ardhi kabla ya ujenzi ni hatua muhimu katika kupunguza changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji au baada ya kukamilika kwa miradi, huku wataalamu wakiwa na uwezo wa kuchagua teknolojia na aina ya ujenzi inayolingana na mazingira ya eneo.
