Featured Kitaifa

MOI YAOKOA SH121.9 BILIONI KWA MATIBABU YA UBINGWA

Written by Alex Sonna

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI), Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya, akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu utekelezaji mwaka wa fedha 2025/2026 na mwelekeo taasisi hiyo kwa mwaka 2026/2027, Septemba 1, 2026 katika ukumbi wa Idara ya Habari – MAELEZO uliopo jengo la Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dodoma.

Na Dotto Kwilasa,Dodoma

TAASISI ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) imeokoa zaidi ya Sh121.99 bilioni ambazo zingetumika nje ya nchi, baada ya kutoa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi kwa wagonjwa 2,282 ndani ya mwaka mmoja, huku ikihudumia jumla ya wagonjwa 211,359 katika mwaka wa fedha 2025/2026.

Akizungumza jijini Dodoma leo Sept 1,2026 wakati akiwasilisha taarifa ya mafanikio ya taasisi hiyo kwa kipindi cha Julai 2025 hadi Juni 2026, Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya, amesema mafanikio hayo yametokana na upanuzi wa huduma za kibingwa, matumizi ya teknolojia za kisasa na kuimarika kwa uwezo wa wataalamu wa ndani.

Amesema hatua hiyo imepunguza utegemezi wa Watanzania kusafiri nje ya nchi kwa matibabu na wakati huohuo imeanza kuifanya Tanzania kuwa kivutio cha huduma za afya kwa wagonjwa kutoka nchi mbalimbali.

Kwa mujibu wa Dkt. Ulisubisya, kati ya wagonjwa 211,359 waliopata huduma katika kipindi hicho, 202,000 walikuwa wa nje (OPD), sawa na wastani wa wagonjwa 18,000 kwa mwezi, huku 9,359 wakilazwa. Alisema MOI pia imepanua huduma zikiwemo upasuaji wa ubongo kwa teknolojia ya kisasa, upasuaji kupitia matundu, tiba ya pingili za mgongo zilizovunjika, kliniki ya tiba ya maumivu, upasuaji rekebishi wa viungo vilivyopooza na kuondoa uvimbe wa ubongo kupitia tundu la pua.

Amesema upanuzi huo umechangia kupunguza rufaa za wagonjwa wa mifupa kwa asilimia 98 na wagonjwa wa ubongo kwa asilimia 97, huku huduma za ubingwa bobezi kama upasuaji wa nyonga, uwekaji wa goti bandia, hydrocephalus na scoliosis zikiendelea kutolewa. Katika upande wa tiba ya mwili (fiziotherapia), MOI ilihudumia wagonjwa 71,819, huku vipimo 83,847 vya radiolojia vikifanyika, vikiwemo MRI 11,533, CT Scan 6,796 na X-Ray 53,384, pamoja na ECG, ECHO na Ultrasound.

Katika kuimarisha tiba utalii, Dkt. Ulisubisya alisema MOI ilihudumia wagonjwa 270 kutoka Comoro, Msumbiji, Malawi, Zambia, Rwanda, Sudan Kusini, Uganda, Burundi, Kenya na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Alisema mvuto huo unatokana na uwepo wa wataalamu wenye uzoefu, vifaa tiba vya kisasa na huduma za kibingwa zinazopatikana nchini, huku kiwango cha kuridhika kwa wagonjwa kikifikia asilimia 87.5 na hatua za kuzuia na kudhibiti maambukizi zikiongezeka kutoka asilimia 70 hadi asilimia 81.

Katika kuimarisha nguvu kazi, MOI ilipandisha vyeo watumishi 199, kubadilisha kada watumishi 15 na kuajiri watumishi wapya 112, huku wataalamu saba wakipelekwa nje ya nchi kwa mafunzo ya ubingwa na ubingwa bobezi. Aidha, kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), taasisi hiyo imeendelea kuwa kituo cha mafunzo kwa wataalamu wa mifupa, mishipa ya fahamu, upasuaji wa ubongo, usingizi na tiba ganzi, pamoja na kuchapisha machapisho 36 ya kisayansi katika majarida ya kimataifa.

MOI pia imeendelea kusogeza huduma karibu na wananchi kupitia huduma mkoba, ambapo wagonjwa 18,455 walihudumiwa, wakiwemo 14,145 waliopata huduma za kliniki na 4,310 waliofanyiwa upasuaji. Wakati huohuo, taasisi hiyo inaendelea na miradi mbalimbali ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya Sh30 bilioni, ikiwemo ujenzi wa jengo jipya la OPD la Sh13.8 bilioni ambalo limefikia asilimia 55 na kutoa ajira kwa vijana zaidi ya 280, pamoja na ukarabati wa MOI Annex wenye thamani ya Sh2.1 bilioni ambao umefikia asilimia 99.

Akizungumzia maandalizi ya Tanzania kwa ajili ya michuano ya AFCON 2027, Dkt. Ulisubisya alisema MOI ipo tayari kutoa huduma za kibingwa kwa wanamichezo na wageni watakaohitaji matibabu, ikiwa na madaktari bingwa bobezi zaidi ya sita katika tiba za michezo. Alisema taasisi hiyo imeandaa kliniki maalum kwa wagonjwa wa kimataifa, vyumba 25 vya kulaza wagonjwa na vifaa vya kisasa ikiwemo MRI, CT Scan, Cathlab, arthroscopic towers, Brain Lab, Digital X-Ray na vifaa vya upasuaji wa ubongo na mgongo, huku huduma za dharura zikiwa tayari.

Katika mipango ya baadaye, MOI imepanga kujenga Kituo cha Matibabu ya Uti wa Mgongo na Urekebishaji wa Viungo katika eneo la Mbweni Mpiji, Dar es Salaam, chenye ukubwa wa ekari 10, kupitia ubia kati ya Serikali na sekta binafsi. Taasisi hiyo pia imepanga kuanza kutoa huduma za OPD katika MOI Annex, Upanga, na kusogeza huduma katika mikoa mbalimbali kupitia programu za outreach na satellite centres. Dkt. Ulisubisya alisema MOI itaendelea kuanzisha huduma mpya za kibingwa na ubingwa bobezi kwa kutumia teknolojia za kisasa, huku ikilenga kupata ithibati za kimataifa na kuimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha huduma za afya barani Afrika.

About the author

Alex Sonna