Na Mwandishi wetu, Dodoma
WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Homera, alisema Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania (LRCT) inapaswa kuharakisha mapitio na maboresho ya sheria mbalimbali ili ziweze kuwezesha utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050, hususan katika uwekezaji na ujenzi wa miundombinu kupitia mfumo wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP).
Dkt. Homera alisema hayo jana jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa Makamishna wapya wa Tume, ufunguzi wa mafunzo elekezi kwa Makamishna hao pamoja na Kikao cha 102 cha Tume hiyo.
Alisema Tume ina jukumu kubwa katika kuhakikisha sheria zinaendana na mahitaji ya Taifa kuelekea utekelezaji wa Dira ya 2050, ikiwemo kuweka mazingira wezeshi katika maeneo ya haki, maendeleo, miundombinu na uwekezaji.
“Tume inayo kazi kubwa sana hasa kuelekea Dira ya 2050 katika utekelezaji wake kwenye masuala ya haki, maendeleo, miundombinu, makampuni, lakini kwenye suala la PPP kuna kazi kubwa inayotakiwa ifanyike,” alisema.
Alisema sheria zinapaswa kufanyiwa marekebisho ili mfumo wa PPP uweze kufanikiwa kwa kiwango kikubwa katika ujenzi wa miundombinu, ikiwemo madaraja, barabara na viwanja vya ndege, pamoja na kuongeza fursa za uwekezaji katika sekta za anga na majini.
Alisema wakati Rais Samia Suluhu Hassan akizindua Dira ya Taifa ya 2050, alisisitiza mambo mbalimbali yanayopaswa kufanyiwa kazi ili kuwezesha maendeleo ya Taifa, ikiwemo kuifanyia kazi mifumo ya sheria inayoweza kuwa kikwazo katika utekelezaji wa Dira hiyo.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, Wizara ya Katiba na Sheria, kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, imepewa jukumu la kufanya mapitio ya sheria zinazohitaji maboresho ili ziendane na utekelezaji wa Dira ya 2050.
Alizitaka Tume hiyo na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuanza kuandaa mapendekezo ya maboresho ya sheria, huku zikishirikisha wizara na taasisi za Serikali pamoja na wadau wa sekta husika.
Dkt. Homera alisema ushirikishwaji huo utasaidia kupata maoni mahsusi kuhusu changamoto zinazotokana na sheria zilizopo kabla ya mapendekezo kuwasilishwa kwa Waziri wa Katiba na Sheria au Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Alisema Tume inapaswa pia kufanya tafiti za kina kuhusu sheria zinazolalamikiwa na wananchi, wafanyabiashara na wadau mbalimbali ili kubaini kama zinahitaji kurekebishwa, kuboreshwa au kuondolewa endapo hazina tena umuhimu katika mazingira ya sasa.
Alizitaja baadhi ya sheria na maeneo yanayohitaji utafiti na mapitio kuwa ni sheria za makampuni, uwekezaji, PPP, kilimo, afya na matumizi ya vilevi pamoja na maeneo mengine mengi.
Aidha, alimtaka Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mwandishi wa Sheria kuweka utaratibu wa kuzikumbusha wizara na taasisi za Serikali kuhakikisha mapendekezo yao ya kutunga au kubadili sheria yanapitia Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania.
Alisema hatua hiyo itasaidia kuhakikisha maboresho ya sheria yanafanyika kwa uratibu na kuzingatia mahitaji ya Taifa, badala ya kila taasisi kufanya mchakato huo kwa namna inayojitegemea.
Waziri huyo pia aliitaka Tume inapofanya tafiti kwa mpango wake yenyewe kuhakikisha inaihusisha Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kuwepo uelewa wa pamoja kuhusu kazi zinazotekelezwa na mapendekezo yanayoandaliwa.
Aidha alisisitiza umuhimu wa Tume kujiwekea muda mahsusi kwa kila mpango kazi wa mapitio ya sheria ili mapendekezo ya maboresho yawasilishwe kwa wakati na kuchangia utekelezaji wa Dira ya 2050.
Awali, Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, Jaji Winfrida Korosso, alisema Tume hiyo ina jukumu muhimu katika maendeleo na uboreshaji wa mifumo ya sheria nchini kwa mujibu wa Sheria ya Tume ya Kurekebisha Sheria, Sura ya 171.
Jaji Korosso alisema miongoni mwa majukumu makuu ya Tume ni kufanya mapitio ya sheria au maeneo ya sheria ili kubaini kasoro, mapungufu na dosari, kupendekeza kuondolewa kwa sheria zilizopitwa na wakati au zisizo na umuhimu, kutoa ushauri kuhusu usimamizi bora wa sheria na utoaji wa haki, pamoja na kutathmini utekelezaji wa sheria ili kubaini kama zinafikia malengo yaliyokusudiwa.
Alisema mafunzo elekezi kwa Makamishna wapya yanalenga kuwawezesha kupata uelewa wa kina wa majukumu yao, kubadilishana uzoefu na Makamishna waliowahi kushika nyadhifa hizo na kujiandaa kutekeleza majukumu yao katika kipindi ambacho Tume inatarajiwa kuwa na nafasi kubwa katika maboresho ya sheria kuelekea Dira ya 2050.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, George Mandepo, alisema Tume imeandaa kikao hicho pamoja na mafunzo elekezi kwa Makamishna wapya ili kuwapatia mbinu na nyenzo zitakazowawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Alisema Tume imejipanga kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050, huku mpango kazi wa mwaka wa fedha 2026/2027 ukijikita katika kufanya utafiti, mapitio, tathmini na kutoa elimu kwa umma kwa mujibu wa majukumu yaliyoidhinishwa na Bunge.
Mandepo alisema Tume pia imejipanga kutekeleza maelekezo yaliyotolewa kuhusu kufanya mapitio ya sheria ili ziendane na mahitaji ya utekelezaji wa Dira ya 2050.
