Featured Kitaifa

MUSWADA WA MABADILIKO YA SHERIA MBALIMBALI KUWEZESHA UTEKELEZAJI WA DIRA YA TAIFA 2050

Written by Alex Sonna

Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Hamza S. Johari amesema kuwa Serikali inaendelea kufanya maboresho katika Sheria mbalimbali ili kuweka mazingira wezeshi ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameyasema hayo tarehe 1 Septemba, 2026 Bungeni Jijini Dodoma, wakati akiwasilisha Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2026 (The Written Laws (Miscellaneous Amendments) Bill, 2026).

Mhe. Johari ameeleza kuwa ili kuyafikia malengo ya Dira ya Taifa 2050 ni muhimu mfumo wa Sheria uendelee kuhuishwa ili kuendana na mabadiliko ya kiuchumi, kijamii, kiteknolojia na kimataifa, kuondoa vikwazo vya utekelezaji na kuimarisha mifumo ya usimamizi.

“Marekebisho ya sheria ni miongoni mwa hatua muhimu za Serikali katika kuweka mazingira wezeshi ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.” Amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Akiwasilisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2026 (The Written Laws (Miscellaneous Amendments) Bill, 2026) Mwanasheria Mkuu wa Serikali amezitaja Sheria zilizofanyiwa maboresho ni pamoja na Sheria ya Kuzuia Utakatishaji wa Fedha Haramu, Sura ya 423, Sheria ya Nguvu za Atomiki, Sura ya 188, Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania, Sura ya 197, Sheria ya Majina ya Biashara, Sura ya 213, Sheria ya Usafiri wa Anga, Sura ya 80, na Sheria ya Kampuni, Sura ya 212.

Aidha, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameeleza pia Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Sura ya 20, Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Sura ya 95, Sheria ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, Sura ya 174, Sheria ya Chuo cha Uhasibu Arusha, Sura ya 240, Sheria ya Tafsiri ya Sheria, Sura ya 1, Sheria ya Usimamizi wa Mahakama, Sura ya 237 na Sheria ya Baraza la Vijana, Sura ya 441.

Vilevile, Mhe. Johari amesema kuwa Muswada huo unapendekeza kufanya maboresho pia katika Sheria ya Usajili wa Hataza, Sura ya 217, Sheria ya Magereza, Sura ya 58, Sheria ya Usimamizi wa Maabara Binafsi za Afya, Sura ya 136, Sheria ya Huduma za Maktaba Tanzania, Sura ya 102, Sheria ya Bodi ya Utalii Tanzania, Sura ya 364, Sheria ya Utalii, Sura ya 65; Sheria ya Alama za Biashara na Huduma, Sura ya 326, na Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, Sura ya 148.

Katika hatua nyingine, Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema kuwa maboresho hayo yaliyofanyika katika sheria hizo yanalenga katika kuimarisha mfumo wa kisheria ili kuoanisha sheria hizo na Dira ya Taifa, 2050.

Sambamba na hilo, Mhe. Johari amesisitiza juu ya umuhimu wa Utawala wa Sheria katika maendeleo ya Taifa, ambapo ameeleza kuwa utawala wa sheria ni msingi muhimu wa kujenga jamii yenye haki, taasisi zinazowajibika na mazingira yenye utulivu yanayowezesha shughuli za kijamii na kiuchumi kustawi.

“Kuendelea kuimarisha utawala wa sheria ni sehemu muhimu ya kuweka msingi wa kufikia malengo ya maendeleo yaliyowekwa katika Dira 2050.” Amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2026 (The Written Laws (Miscellaneous Amendments) Bill, 2026), umejadiliwa kisha kupitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na upalekwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya kusainiwa na kuwa Sheria kamili.

About the author

Alex Sonna