Featured Kitaifa

DKT. MSENGWA: SAYANSI YA DATA NA AI KUONGEZA UFANISI WA TAKWIMU NCHINI

Written by Alex Sonna

 

Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Amina Msengwa,akizungumza  wakati wa hafla ya utiaji saini Hati ya Makubaliano (MoU) kati ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Arusha (NM-AIST), yenye lengo la kuimarisha matumizi ya teknolojia katika uzalishaji wa takwimu rasmi.hafla iliyofanyika leo Agosti 22,2026 jijini Dodoma.

….

Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Amina Msengwa, amesema matumizi ya Sayansi ya Data, Akili Mnemba (AI) na vyanzo vipya vya taarifa yataongeza ufanisi katika uzalishaji wa takwimu rasmi nchini na kusaidia Serikali kupata majibu ya maswali mbalimbali ya maendeleo.

Ameyasema hayo Agosti 22, 2026 Jijini Dodoma , wakati wa hafla ya utiaji saini Hati ya Makubaliano (MoU) kati ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Arusha (NM-AIST), yenye lengo la kuimarisha matumizi ya teknolojia katika uzalishaji wa takwimu rasmi.

Amesema ushirikiano huo utaiwezesha NBS kutumia vyanzo vya kawaida na visivyo vya kawaida vya takwimu, ikiwemo taarifa za kiutawala na taarifa zinazopatikana kwenye mifumo ya kidijitali, huku wataalamu kutoka vyuo vikuu wakisaidia katika uchambuzi, uundaji wa mifumo na matumizi ya Sayansi ya Data na AI.l

“Tunatakiwa kuunganisha traditional na non-traditional data sources. Hii inaleta tija kubwa sana, kwa sababu tunapokusanya takwimu tu haitoshi kama hatutazichambua na kuzitumia kutoa majibu,” amesema Dkt. Msengwa.

Amesema MoU hiyo pia inalenga kuimarisha uwezo wa wataalamu kupitia mafunzo na kubadilishana uzoefu katika maeneo ya Data Science na Artificial Intelligence, hatua ambayo itasaidia kujenga rasilimali watu yenye uwezo wa kukabiliana na mahitaji mapya ya uzalishaji na uchambuzi wa takwimu.

Aidha, Dkt. Msengwa amesema ushirikiano huo utaimarisha Data Analytics na maabara za takwimu, huku wataalamu kutoka taasisi hizo wakishirikiana kutengeneza ubunifu na suluhisho zitakazowasaidia watunga sera, Serikali na wafanyabiashara kufanya maamuzi sahihi, ikiwemo kujua maeneo yenye fursa za uwekezaji.

Amesema makubaliano hayo yameandaliwa kwa kuzingatia uwezo na utaalamu wa kila taasisi, huku NBS ikiwa na jukumu la kuhakikisha takwimu zinazozalishwa zinazingatia vigezo na metodolojia zinazoaminika kitaifa na kimataifa na kuchangia katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya nchi.

Aidha, amesisitiza kuwa utekelezaji wa MoU hiyo hautahitaji kusubiri muda mrefu, akibainisha Kuwa NBS iko tayari kushirikiana na UDSM pamoja na NM-AIST kuhakikisha suluhisho za maswali mbalimbali zinapatikana kwa wakati, ikiwemo ndani ya wiki mbili, miezi miwili au miezi minne kutegemea ukubwa wa kazi husika.

Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo cha NM-AIST, Prof. Maulilio John Kipanyula, amesema maamuzi makubwa ya taifa hayawezi kujengwa kwa hisia au makisio, bali yanahitaji takwimu sahihi, ushahidi wa kisayansi pamoja na uwezo wa kufanya modeling, simulations na predictions.

Ameongeza Kuwa ushirikiano kati ya NBS, UDSM na NM-AIST una uwezo wa kuchangia moja kwa moja katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa kusaidia taifa kupanga na kufanya maamuzi kwa uhakika zaidi.

About the author

Alex Sonna