Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi akiwa kwenye picha na Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo Taifa Mhe. Othman Masoud Othman baada ya kushuhudia utiaji saini wa ajenda zilizokubaliwa na pande zote mbili kwa ajili ya kufanyiwa kazi kufuatia Tamko la Pamoja la Muafaka wa Kisiasa baina ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na ACT-Wazalendo, katika viwanja vya Ikulu Zanzibar tarehe 09 Julai, 2026.
….
Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Taifa, Othman Masoud Othman, amesema maridhiano yaliyofikiwa Zanzibar ni hatua muhimu katika kutafuta suluhu ya changamoto za kisiasa, huku akibainisha kuwa wananchi wamegawanyika katika mitazamo mitatu kuhusu mchakato huo.
Akizungumza baada ya kusainiwa kwa Tamko la Maridhiano ya Zanzibar, Othman amesema kundi la kwanza linajumuisha viongozi na wananchi walioupokea mchakato huo kwa matumaini makubwa, wakiamini kuwa ni njia sahihi ya kujenga maridhiano ya kudumu na kwamba viongozi wanaousimamia watautekeleza kwa uaminifu.
Amesema kundi la pili linaundwa na wananchi waliopoteza imani kutokana na uzoefu wa matukio ya nyuma, hivyo bado wana mashaka kuhusu mafanikio ya mchakato huo.
Aidha, amesema kundi la tatu ni la watu wanaopinga maridhiano pamoja na wazo la kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), wakidai kuwa hatua hiyo haitaleta mabadiliko yenye manufaa kwa Zanzibar.
“Kibaya zaidi, wanapinga mchakato huu kwa kisingizio kwamba Zanzibar ni nchi ya kimapinduzi, hivyo inapaswa kuendeshwa kimapinduzi. Kana kwamba madhumuni ya mapinduzi ni fujo, vurugu, ufisadi na kutokuwepo kwa sheria na taratibu,” amesema Othman.
Amesisitiza kuwa maridhiano yanapaswa kupewa nafasi kama njia ya kujenga umoja, kuimarisha utulivu wa kisiasa na kuweka msingi wa maendeleo endelevu ya Zanzibar.