Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel akizungumza na wageni waalikwa wakati wa hafla ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na benki ya NBC kwa ajili ya wateja wadogo na wakubwa wa jijini Mwanza hivi karibuni ili kujadili fursa za biashara na kutambulisha huduma mpya za benki hiyo.
Mkuu wa Kitengo cha Wajasiriamali wa Benki ya NBC hiyo Bw Mussa Mwinyidaho akizungumza na wageni waalikwa wakati wa hafla ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na benki hiyo kwa ajili ya wateja wadogo na wakubwa wa jijini Mwanza hivi karibuni ili kujadili fursa za biashara na kutambulisha huduma mpya za benki hiyo.
Baadhi ya wateja wa benki ya NBC jijini Mwanza wakiwa kwenye hafla hiyo.
……………………………………
Na Mwandishi Wetu,Mwanza
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel hivi karibuni aliungana maofisa waandamizi wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) kuwafunda wafanyabiashara wakubwa na wadogo wa jijini Mwanza wakilenga kuwapa ujuzi wa jinsi ya kukuza biashara zao kwa maendeleo yao na taifa kwa ujumla.
Akizungumza wakati wa hafla ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na benki ya NBC kwa ajili ya wateja wadogo na wakubwa wa jijini humo mwishoni mwa wiki, Mhandisi Gabriel aliwashauri wafanyabiashara hao kuhakikisha wanatumia vema huduma za kifedha zinazotolewa na Benki ya NBC kukuza mitaji yao ili kujiongezea faida zaidi.
“Kikubwa ni kuhakikisha tu kwamba kila unachokifikiria kukifanya kuhusu biashara ukifikirie kwa ukubwa wake. Kama ni biashara ya duka basi hakikisha unafungua duka kubwa lenye huduma nzuri na za kisasa ili uweze kuvutia na kuhudumia wateja wengi iwekanavyo ili kukuza mtaji wako lakini pia uweze kuvutia taasisi za kifedha zishawishike kuendelea kukuunga mkono,’’ alisema
Hafla hiyo ilienga kujadili fursa za biashara na kutambulisha huduma mpya za benki hiyo kupitia klabu yake Biashara inayofahamika kama NBC Business Club,
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Wajasiriamali wa Benki hiyo Bw Mussa Mwinyidaho alisema benki hiyo imedhamiria kuboresha huduma zaidi ili wateja wake waendelee kufurahia huduma zilizorahisishwa zaidi ili kuendana na matakwa ya shughuli zao ili waweze kukuza biashara zao.
“Ni kutokana na ubunifu wa huduma na fursa mpya kila mara ndio sababu tumekuwa na huu utaratibu wa kukutana na nyinyi wateja wetu ili kuwasilisha kwenu huduma hizi mpya. Kupitia huduma yetu ya NBC Business ClUB tunaweza kutangaza huduma mpya kwa ajili ya wajasiriamali ikiwemo huduma ya ‘Commercial Property Financing’ inayowawezesha wajasiriamali wenye majengo ya biashara kupata mikopo yenye marejesho nafuu sambamba na huduma ya ‘Commercial Asset Financing’ inayowawezesha wajasiriamali hao kukopa mitambo kwa ajili ya biashara na shughuli za ukandarasi.’’
“Pia kupitia tukio hili la leo wateja wetu jijini Mwanza watapata fursa ya kufahamu huduma zetu za mikopo bila dhamana ikiwepo huduma ya ‘Distributor financing’ inayowawezesha wajasiriamali kupata mikopo ya kusambaza bidhaa zao bila dhamana pamoja na huduma ya ‘Purchasing Order Financing’ inayowawezesha wajasiriamali kupata mikopo kwa kutumia Hati ya manunuzi yaani LPO ,’’ alisema.