Featured • Kitaifa

BAJETI YA WIZARA YA MAJI YAPAA,ASILIMIA  93 KWENDA KATIKA MIRADI YA MAJI 

Written by Alex Sonna

Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso, akiwasilisha Hotuba ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 leo Mei 5,2026 bungeni Dodoma.

Na.Alex Sonna,Mzalendo blog-DODOMA

Serikali imeongeza bajeti ya Wizara ya Maji kutoka Sh bilioni  898.2 mwaka 2025-2026  hadi kufikia Sh trilioni 1.12 ambapo zaidi ya asilimia 93 zitaenda katika miradi ya Maji.

Fedha hizo ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi, sambamba na kuboresha huduma za usafi wa mazingira nchini.

Kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni  80.7 sawa na asilimia 7 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na  Sh trilioni 1.04   sawa na asilimia 93 ni fedha za maendeleo zitakazotumika kutekeleza miradi mbalimbali ya maji nchini.

Akiwasilisha leo Mei 5,2026  makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo Kwa mwaka wa fedha 2026-2027  bungeni, Waziri wa Maji,Jumaa Aweso amesema  kuwa katika mwaka wa fedha 2025/26 wizara iliidhinishiwa jumla ya Shilingi bilioni 898.2  ambapo kati ya fedha hizo zaidi ya Shilingi bilioni 824 zilielekezwa kwenye miradi ya maendeleo huku sehemu iliyobaki ikitumika kwa matumizi ya kawaida. 

Amesema  hadi Aprili 2026, zaidi ya asilimia 83 ya bajeti hiyo ilikuwa imeshapokelewa na kuelekezwa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji nchini. 

Waziri Aweso amesema  katika mwaka 2026/27, Wizara hiyo imeomba kuidhinishiwa zaidi ya Sh trilioni 1.12 Kwa ajili ya kutekeleza Vipaumbele sita.

Amesema  kati ya fedha hizo, Shilingi 80.6  sawa na asilimia 7 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida, ambapo Shilingi 1.039 sawa na asilimia 93 ni fedha za maendeleo zitakazotumika kutekeleza miradi mbalimbali ya maji nchini.

About the author

Alex Sonna