Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yussuf Masauni akizungumza katika ufunguzi wa Mkutano wa Masoko ya Kaboni Afrika wa mwaka 2026 unaofanyika kwa siku mbili Kigali nchini Rwanda, kuanzia Oktoba 14, 2026.
NA; MWANDISHI WETU,KIGALI, RWANDA
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, amesema Tanzania imepiga hatua katika kuendeleza masoko ya kaboni, huku miradi sita ikifikia hatua ya kuzalisha krediti za kaboni, hatua inayofungua fursa zaidi za uwekezaji wa kijani, uhifadhi wa mazingira na kuboresha maisha ya wananchi.
Masauni ameyasema hayo Oktoba 14, 2026, jijini Kigali, Rwanda, wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Masoko ya Kaboni Afrika wa mwaka 2026, unaowakutanisha viongozi wa Serikali, wawekezaji, wanunuzi wa krediti za kaboni, waendelezaji wa miradi na taasisi za kifedha za maendeleo kutoka maeneo mbalimbali.
Amesema maendeleo hayo yanaonesha hatua zinazopigwa na Tanzania katika kujenga soko la kaboni lenye mifumo madhubuti ya usimamizi, uwazi na uadilifu, huku likilenga kuchangia juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kukuza maendeleo endelevu.
Ameeleza kuwa katika kikao cha mwisho cha Kamati ya Taifa ya kutathmini miradi ya kaboni, miradi minne iliyofikia hatua ya ukomavu na inayohusisha nishati safi ya kupikia pamoja na manufaa ya kijamii iliidhinishwa, hatua iliyochangia kuisogeza mbele katika mchakato wa kuzalisha krediti za kaboni zinazoweza kuthibitishwa.
“Serikali imeendelea kuimarisha mifumo ya kisera na kitaasisi inayosimamia shughuli za biashara ya kaboni ili kuhakikisha miradi inayotekelezwa inatoa matokeo chanya katika uhifadhi wa mazingira na kuleta manufaa yanayoonekana kwa wananchi.”
“Kupitia marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2025, Serikali imeanzisha Kituo cha Taifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC), chenye jukumu la kusajili miradi, kusimamia upimaji na uhakiki wa matokeo pamoja na kuzuia kuhesabiwa mara mbili kwa matokeo ya miradi ya biashara ya kaboni.” Amesema Masauni.
Akizungumzia fursa za soko la kaboni barani Afrika, Masauni amezitaka nchi za Afrika kutumia mkutano huo kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, wawekezaji, wanunuzi, waendelezaji wa miradi na taasisi za kifedha za maendeleo ili kuharakisha utekelezaji wa miradi yenye manufaa ya kimazingira.
Amesema ni muhimu kuunganisha miradi yenye viwango vya ubora na mahitaji halisi ya soko, kuhakikisha upatikanaji wa mitaji ya muda mrefu, kuimarisha mifumo ya upimaji na uthibitishaji wa matokeo na kuhakikisha wananchi wanafaidika na mapato na fursa zinazotokana na miradi hiyo.
Masauni amesisitiza pia umuhimu wa nchi za Afrika kujenga uwezo wa kitaalamu na kiuongozi katika sekta ya kaboni ili ziweze kushiriki kikamilifu katika soko la kimataifa, pamoja na kuwa na nafasi ya kuchangia maamuzi kuhusu mwelekeo, kanuni na viwango vya soko hilo.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Kituo cha Taifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC), Kathryn Kigaraba, amesema mkutano huo ni jukwaa muhimu la kuwakutanisha wadau wa sekta ya kaboni ili kujadili namna ya kuimarisha mazingira ya uwekezaji, kuongeza utekelezaji wa miradi na kujenga soko lenye uaminifu na manufaa kwa jamii.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dkt. Immaculate Semesi amesema NEMC itaendelea kushirikiana kwa karibu na Kituo cha Taifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC) kusimamia na kufanikisha miradi ya kaboni ili ilinde Mazingira na kuwanufaisha wananchi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yussuf Masauni akisalimiana na Waziri wa Mazingira wa Rwanda Dkt. Bernadette Arakwiye mara baada ya ufunguzi wa Mkutano wa Masoko ya Kaboni Afrika wa mwaka 2026 unaofanyika kwa siku mbili Kigali nchini Rwanda, kuanzia Oktoba 14, 2026.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yussuf Masauni (katikati), Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dkt. Immaculate Semesi (kulia) na Afisa Mtendaji Mkuu wa Kituo cha Taifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC), Kathryn Kigaraba wakizungumza mara baada ya ufunguzi wa Mkutano wa Masoko ya Kaboni Afrika wa mwaka 2026 unaofanyika kwa siku mbili Kigali nchini Rwanda, kuanzia Oktoba 14, 2026.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yussuf Masauni (wa nne kutoka kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Mawaziri na viongozi mbalimbali mara baada ya ufunguzi wa Mkutano wa Masoko ya Kaboni Afrika wa mwaka 2026 unaofanyika kwa siku mbili Kigali nchini Rwanda, kuanzia Oktoba 14, 2026.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yussuf Masauni (katikati) akishiriki Mkutano wa Masoko ya Kaboni Afrika wa mwaka 2026 unaofanyika kwa siku mbili Kigali nchini Rwanda, kuanzia Oktoba 14, 2026.