Featured Kitaifa

AAPAM YAWAITA WATUMISHI WA UMMA MKUTANO MKUU ARUSHA KUJADILI MABORESHO YA HUDUMA KWA WANANCHI

Written by Alex Sonna

 

Mwenyekiti wa AAPAM Tawi la Tanzania , Bi. Leila Mavika, ametangaza kufanyika kwa Mkutano Mkuu wa Pili wa Mwaka wa Jumuiya ya Wataalamu wa Usimamizi wa Rasilimaliwatu na Utawala katika Utumishi wa Umma, utakaoanza Mei 5 hadi 8, 2026 jijini Arusha.

Akizungumza na waandishi wa habari Aprili 28, 2026, Bi. Mavika amesema mkutano huo unalenga kuwakutanisha wataalamu wa utawala wa umma na usimamizi wa rasilimaliwatu ili kujadili mbinu bora za kuboresha utendaji kazi na utoaji wa huduma kwa wananchi.

Amesema mkutano huo utaongozwa na kaulimbiu isemayo “Kufikiri upya utoaji wa huduma kwa Umma: Jinsi Serikali inavyoweza kutumia Teknolojia kuanzisha huduma bora na zinazolenga wananchi, kukabiliana na ukosefu wa ajira kwa vijana na changamoto za mazingira.”

Bi. Mavika ameeleza kuwa mkutano huo umeandaliwa kwa ushirikiano kati ya AAPAM Tanzania Chapter, Tanzania Association for Public Administration and Human Resources (TAPAHR) na TPS-HRMnet, ambapo washiriki watapata fursa ya kujadili changamoto mbalimbali zinazokabili kada hiyo na kutafuta suluhisho la pamoja.

Ameongeza kuwa mada mbalimbali zitawasilishwa na wataalamu wabobezi katika utumishi wa umma, zikiwa na lengo la kuongeza ufanisi, tija na ubunifu katika sekta ya umma nchini.

Aidha, amesema mgeni rasmi katika mkutano huo anatarajiwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Jakaya Kikwete.

Katika hatua nyingine, Bi. Mavika amewashukuru waajiri ambao tayari wamewezesha watumishi wao kushiriki mkutano huo na kutoa wito kwa taasisi ambazo bado hazijafanya hivyo kuhakikisha zinawawezesha wataalamu wao kuhudhuria ili kujengewa uwezo zaidi.

Amesema siku ya mwisho ya mkutano, Mei 8, 2026, washiriki watapata nafasi ya kushiriki zoezi la kuimarisha mshikamano (team building) katika Ngorongoro National Park.

Ametoa wito kwa watumishi wa umma kujitokeza kwa wingi na kujisajili kabla ya Mei 1, 2026 ili kushiriki mkutano huo muhimu unaotarajiwa kuongeza ubora wa huduma kwa wananchi nchini.



About the author

Alex Sonna