Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana Mhe. Joel Nanauka,akiwasilisha Hotuba ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 leo Aprili 20,2026 bungeni jijini Dodoma.
Na.Alex Sonna,Mzalendo blog-DODOMA
Serikali imetangaza mkakati kabambe wa shughuli zitakazotekelezwa katika mwaka wa fedha 2026/27, ukilenga kubadili sura ya maisha ya vijana nchini kwa kuwapa nafasi kubwa zaidi katika uchumi, uongozi na maendeleo ya jamii.
Hayo yameelezwa leo Aprili 20,2026 bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana Mhe. Joel Nanauka,akiwasilisha Hotuba ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027.
Amesema , shughuli hizo zinatokana na vipaumbele vya kitaifa vinavyolenga kuimarisha ushirikishwaji wa vijana pamoja na kuwawezesha kiuchumi na kijamii.
“Wizara imepanga kuanzisha Mfumo wa Taifa wa kuratibu maendeleo ya vijana, pamoja na kuunda Kanzidata ya kitaifa itakayokusanya taarifa muhimu za vijana kote nchini. Hatua hii inalenga kuweka msingi wa maamuzi sahihi ya sera na mipango ya maendeleo.”amesema Mhe.Nanauka
Aidha, amesema mapitio ya Sheria ya Baraza la Vijana la Taifa yamepangwa kufanyika ili kuendana na mahitaji ya kizazi cha sasa, huku Mkakati wa Kitaifa wa Vijana, Amani na Usalama ukiandaliwa ili kuwapa vijana nafasi katika ajenda za amani ndani na nje ya nchi. Vijana pia watawezeshwa kushiriki katika majukwaa ya kikanda na kimataifa, hatua inayotarajiwa kupanua upeo wao na kuongeza mchango wao katika masuala ya kimataifa.
Katika kukuza uzalendo, Serikali itaendelea kuratibu elimu ya uraia katika halmashauri zote nchini pamoja na kuendesha matukio ya kitaifa kama mbio za Mwenge wa Uhuru na wiki ya vijana. Maadhimisho ya siku muhimu za vijana kitaifa na kimataifa pia yatapewa kipaumbele ili kujenga kizazi chenye maadili na uwajibikaji.
Kwa upande wa ustawi wa vijana, Wizara imejipanga kuanzisha programu maalum za kushughulikia changamoto zinazowakabili vijana, ikiwemo afya ya akili. Mwongozo wa kitaifa wa msaada wa kisaikolojia utaandaliwa ili kuhakikisha vijana wanapata huduma stahiki katika kukabiliana na msongo wa mawazo na changamoto za maisha ya kisasa.
Katika sekta ya uchumi, msisitizo mkubwa umewekwa kwenye ujasiriamali na uwezeshaji wa vijana. Serikali itaendelea kutoa mafunzo ya biashara na ujuzi wa usimamizi, pamoja na mikopo nafuu kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana. Vituo vya mafunzo vya Sasanda, Ilonga na Marangu vitakarabatiwa ili kuongeza upatikanaji wa ujuzi unaohitajika katika soko la ajira, hususan katika kilimo biashara na TEHAMA.
Mpango wa kuanzisha vituo vya ubunifu kwa vijana (VIJANA Hub) nao umepewa uzito mkubwa. Vituo hivi vitasaidia kukuza mawazo ya biashara, kuendeleza vipaji na kuwaunganisha vijana na fursa za masoko, mitaji na teknolojia.
Katika hatua inayotazamwa kama ya kihistoria, Serikali imeanza utafiti wa kuanzisha Benki ya Vijana. Benki hiyo inalenga kutoa huduma za kifedha zinazolenga moja kwa moja mahitaji ya vijana, hasa wale wanaoanza shughuli za kiuchumi. Inatarajiwa kusaidia kuondoa changamoto za upatikanaji wa mitaji na kuongeza uwekezaji wa vijana katika sekta mbalimbali.
Kwa ujumla, mpango huu unaashiria mwelekeo mpya wa kuwajengea vijana mazingira bora ya kufanikiwa, huku ukiweka msingi wa taifa lenye nguvu kazi yenye ubunifu, ujuzi na uzalendo.