Featured Kitaifa

SERIKALI YAWEKA MSUKUMO MPYA KWA VIJANA NCHINI 2026/27

Written by Alex Sonna

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana Mhe. Joel Nanauka, akiwasilisha Hotuba ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 leo Aprili 20,2026 bungeni Dodoma.

Na.Alex Sonn,Mzalendo blog-DODOMA

Katika jitihada za kukabiliana na changamoto za ajira na kuongeza mchango wa vijana katika maendeleo ya taifa, Serikali kupitia Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana imetangaza vipaumbele vya mpango wake kwa mwaka wa fedha 2026/27, vikilenga kuibua fursa, kuimarisha ushiriki na kukuza ustawi wa vijana nchini.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana Mhe. Joel Nanauka, akiwasilisha Hotuba ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 leo Aprili 20,2026 bungeni Dodoma.

Mhe.Nanauka amesema kuwa kipaumbele kikubwa kitawekwa katika kuimarisha ukuzaji wa biashara na uwezeshaji wa vijana kiuchumi. Hatua hiyo inalenga kuwajengea vijana uwezo wa kujiajiri na pia kuajiriwa katika sekta mbalimbali za biashara na uzalishaji. Wachambuzi wa masuala ya maendeleo wanaona hili kama suluhisho muhimu katika kupunguza tatizo la ajira kwa vijana ambalo limekuwa likiikabili nchi kwa muda mrefu.

“Serikali imekusudia kuimarisha uratibu na ushirikishaji wa vijana katika masuala ya kijamii, kiuchumi na kisiasa. Kupitia hatua hiyo, vijana wanatarajiwa kushiriki kikamilifu katika michakato ya maamuzi, jambo litakalosaidia kuibua mawazo mapya na kuongeza uwajibikaji katika jamii.”amesema Mhe.Nanauka

Katika kuendeleza misingi ya taifa, mpango huo pia umeweka mkazo katika kuimarisha elimu ya uraia na uzalendo, pamoja na kuratibu vyema shughuli za Mwenge wa Uhuru. Lengo ni kuwajenga vijana wenye maadili, wanaoipenda nchi yao na wanaoshiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya kitaifa.

Aidha, ustawi na makuzi ya vijana umepewa uzito maalum. Serikali inalenga kuboresha mazingira ya ukuaji wa vijana kwa kuhakikisha wanapata huduma bora za kijamii, msaada wa kisaikolojia, pamoja na fursa za kujifunza na kuendeleza vipaji vyao.

Kwa ujumla, vipaumbele hivi vinaonekana kuwa dira muhimu ya kuleta mageuzi chanya kwa vijana, ambao ndio nguvu kazi kubwa ya taifa. Utekelezaji wake utaamua kwa kiasi kikubwa mustakabali wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.

About the author

Alex Sonna