Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, akiwasilisha Hotuba ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 leo Aprili 17,2026 bungeni Dodoma.
Na.Alex Sonna,Mzalendo blog-DODOMA
Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Tume ya Utumishi wa Umma imeweka wazi mpango wake wa mwaka wa fedha 2026/27, unaolenga kuimarisha uwajibikaji, haki za watumishi na usimamizi wa sheria katika Utumishi wa Umma nchini.
Hayo yamesemwa leo Aprili 17,2026 bungeni Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, akiwasilisha Hotuba ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027.
Amesema kuwa Tume itafanya mikutano minne ya kisheria itakayoshughulikia na kutoa uamuzi kuhusu rufaa, malalamiko na masuala mbalimbali ya kiutumishi, ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati na kwa mujibu wa sheria.
Katika kusimamia uzingatiaji wa sheria na taratibu, Tume imepanga kufanya ukaguzi wa kawaida katika taasisi 300 za umma pamoja na ukaguzi maalum katika taasisi 10, ili kubaini namna Sheria, Kanuni na Miongozo ya usimamizi wa rasilimaliwatu inavyotekelezwa.
Aidha, taasisi 574 za utumishi wa umma zitapatiwa elimu kuhusu majukumu ya Tume na umuhimu wa kuzingatia taratibu za kiutumishi, hatua inayolenga kupunguza migogoro na kuongeza ufanisi katika utendaji kazi.
Katika kuimarisha mifumo ya kidijitali, Tume itaendeleza maboresho ya Mfumo wa Kielektroniki wa Kushughulikia Rufaa na Malalamiko (PSCMIS), ambao unalenga kuongeza kasi na ufanisi katika utoaji wa haki kwa watumishi wa umma.
Vilevile, Tume itafuatilia na kuhakiki vielelezo vya rufaa na malalamiko kutoka kwa warufani na mamlaka za nidhamu ili kuhakikisha maamuzi yanayotolewa yanazingatia ushahidi na sheria zilizopo.
Katika kuimarisha ushirikiano wa kikanda, Tume ya Utumishi wa Umma itaendelea kushirikiana na tume nyingine barani Afrika na ndani ya ukanda wa SADC, kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kuimarisha mifumo ya utumishi wa umma.
Pia, Tume itaendeleza ushirikiano na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali katika kushughulikia mashauri ya kisheria yanayohusu watumishi wa umma yanayofikishwa mahakamani, ili kuhakikisha utetezi na ufafanuzi wa hoja unafanyika kwa ufanisi.
Kwa mwaka wa fedha 2026/27, Tume ya Utumishi wa Umma imeomba kuidhinishiwa jumla ya shilingi bilioni 12.86, ambapo asilimia 96.11 zitatumika kwa matumizi ya kawaida na asilimia 3.89 zitaelekezwa kwenye miradi ya maendeleo.
Kwa ujumla, mpango huu unaonesha dhamira ya Serikali ya kuimarisha haki, uwajibikaji na ufanisi katika Utumishi wa Umma kupitia usimamizi thabiti wa sheria na mifumo ya kisasa ya utendaji.