Na WMJJWM New York Marekani
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesisitiza mshikamano wake na nchi wanachama wa jumuiya ya kimataifa katika kuendeleza ajenda ya usawa wa kijinsia duniani.
Akizungumza katika mkutano wa 70 wa kimataifa kuhusu masuala ya wanawake na haki, mwakilishi wa Tanzania katika Mkutano huo Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makuundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amesema Tanzania inasisitiza kuwa upatikanaji wa haki ni msingi muhimu wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Aidha, amesema Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 imeweka usawa wa kijinsia na ujumuishi wa kijamii kuwa nguzo kuu za ajenda ya maendeleo ya taifa, hali inayotumika kuongoza maboresho ya sheria na sera mbalimbali nchini.
Ameongeza kuwa Serikali imeendelea kutunga na kutekeleza sheria muhimu zinazolenga kulinda haki za wanawake na watoto wa kike. Baadhi ya sheria hizo ni pamoja na Sheria ya Ardhi, Sheria ya Msaada wa Kisheria, Sheria ya Ardhi ya Vijiji, Sheria ya Mtoto, Sheria ya Elimu pamoja na Kanuni ya Adhabu. Sambamba na hilo, mfumo wa mahakama umeimarishwa ambapo Tanzania imefanikiwa kupunguza kwa asilimia 50 mrundikano wa mashauri ya rufaa kati ya mwaka 2021 na 2024.
“Kupitia mageuzi ya kisheria, Tanzania imedhibiti mila na desturi zenye ubaguzi na kufanya marekebisho ya sheria mbalimbali ikiwemo Sheria za Uchaguzi ili kufanya unyanyasaji wa kijinsia katika siasa kuwa kosa la jinai. “amesema Dkt. Gwajima
Pia Dkt. Gwajima amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeanzisha Mkakati wa Kitaifa wa Wanawake kupata Haki, Mkakati wa Pili wa Miaka Mitano wa Haki kwa Watoto, Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto, pamoja na Sera ya Taifa ya Ardhi inayohakikisha haki za wanawake kurithi ardhi huku juhudi zikiendelea kuimarishwa ili kutokomeza vitendo vya ukatili na mila potofu kama ukeketaji na ndoa za utotoni.
Dkt. Gwajima ameeleza kuwa katika kuboresha upatikanaji wa haki na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma za sheria, Tanzania imeanzisha ubunifu mbalimbali ikiwemo mfumo wa usimamizi wa mashauri kwa njia ya kielektroniki (e-Case Management), Vituo Jumuishi vya Haki, pamoja na vituo maalum vya huduma za pamoja (One Stop Centres). Mwaka 2025, asilimia 88 ya mashauri katika vituo hivyo yalitatuliwa, huku wanawake wakichangia asilimia 61 ya wanufaika wa huduma za msaada wa kisheria.
Amefafanua kuwa kupitia Kampeni ya Kitaifa ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, zaidi ya wanawake na wasichana milioni 2.1 Tanzania wamepatiwa msaada wa kisheria, elimu ya sheria pamoja na uwakilishi mahakamani.
Pamoja na mafanikio hayo, Tanzania imesisitiza kuwa bado kuna kazi kubwa ya kufanya katika kuhakikisha usawa wa kijinsia na upatikanaji wa haki kwa wote. Hivyo, imezitaka nchi na wadau wa maendeleo kuimarisha ushirikiano na ushirikishwaji ili kuendeleza ajenda ya kimataifa ya usawa wa kijinsia. Tanzania imeeleza kuwa iko tayari kujifunza kutoka kwa wengine na kushirikiana kwa pamoja katika kufanikisha lengo hilo duniani.
