Arumeru, Arusha
Wananchi wa kata ya Tengeru katika Halmashauri ya wilaya ya Meru wameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kujenga barabara za lami zenye urefu wa Km 4.2 katika eneo hilo, hatua iliyosaidia kupunguza changamoto ya usafiri na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, viongozi na wananchi wa kata hiyo wameeleza kuwa ujenzi wa barabara hizo umefungua fursa mpya za biashara, utalii pamoja na elimu katika eneo hilo ambalo kwa miaka mingi lilikuwa linakabiliwa na changamoto ya miundombinu mibovu ya barabara.
Diwani wa kata ya Akheri Mhe. Julius Mungure amesema wanamshukuru Rais kwa namna alivyoipendelea kata yao kwani changamoto kubwa iliyokuwa ikiwasumbua kwa muda mrefu ilikuwa ni ubovu wa barabara.
Amesema kwa sasa kata hiyo imepata barabara tatu za lami ambazo zimekuwa msaada mkubwa kwa wananchi na wadau wa maendeleo.
“Barabara hizi ni muhimu sana kwa kuwa katika eneo hili kuna masoko matatu, taasisi zaidi ya 10 pamoja na hoteli za kitalii na maeneo ya utalii, huku zikitumiwa na wananchi zaidi ya 10,000. Kwa muda mrefu tulikuwa na changamoto kubwa ya barabara, lakini sasa tunashukuru serikali kwa kutujengea barabara zenye kiwango kizuri,” amesema.
Ameongeza kuwa uboreshaji wa miundombinu hiyo umeanza kuleta matokeo chanya kwani wananchi wengi sasa wanaendelea kuwekeza katika shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Amesema awali watalii wengi walishindwa kufika katika eneo hilo kutokana na ubovu wa barabara, lakini kwa sasa idadi ya watalii imeanza kuongezeka huku taasisi mbalimbali zikiendelea kujengwa.
Aidha, ameahidi kushirikiana na wananchi kuhakikisha barabara hizo zinalindwa na kudumishwa katika hali ya usafi na ubora wakati wote.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Soko la Tengeru Bw. Johnson Msangi, ameishukuru Serikali kupitia TARURA) kwa ujenzi wa barabara hiyo, akisema imewarahisishia wafanyabiashara kuingiza magari sokoni na hivyo kupunguza gharama za kusafirisha mazao kufikisha sokoni.
Amesema ujio wa barabara hiyo umeanza kuleta mafanikio katika wilaya ya Arumeru kwa kuwa usafirishaji wa bidhaa umeboreshwa na gharama zilizokuwa zikitumika hapo awali zimepungua kwa kiasi kikubwa.
“Kwa kweli wafanyabiashara wengi wa kata ya Tengeru tunashukuru sana. Hata wakati wa mvua nyingi barabara hii inapitika tofauti na ilivyokuwa hapo awali. Tunamshukuru sana Rais Samia pamoja na TARURA kwa kutujengea barabara hii ambayo imeondoa changamoto kubwa kwa wafanyabiashara wa soko hili,” amesema.
Bw. Msangi ameongeza kuwa barabara hiyo imejengwa pamoja na mifereji ya maji, hivyo wafanyabiashara wameanza kujipanga kuhamasishana kulinda miundombinu hiyo kwa kuhakikisha mazingira yanakuwa safi wakati wote.
Amesema pia wafanyabiashara wanatarajia kuweka vyombo vya kuhifadhia taka ili kufanya soko la Tengeru na maeneo yanayozunguka kuwa safi na kuvutia wageni, hususan watalii wanaopita katika hoteli mbalimbali zilizopo katika eneo hilo.
Naye, Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Juu ya Maendeleo ya Jamii Tengeru, Bw. Bakari George, ameishukuru serikali ya Awamu ya Sita kwa maono yake ya kujenga na kukamilisha barabara hiyo ya lami ambayo imeondoa changamoto kubwa ya usafiri kwa wanafunzi na watumishi wa taasisi hiyo.
Amesema kwa miaka mingi barabara hiyo ilikuwa katika hali mbaya na haikuchochea maendeleo ya chuo pamoja na uchumi wa maeneo ya jirani.
“Kwa muda mrefu barabara hii ilikuwa kikwazo kikubwa. Wanafunzi waliokuwa wanasoma katika ngazi za chini hawakuwa na hamasa ya kuendelea na masomo ya juu kutokana na changamoto ya miundombinu. Lakini sasa hali imebadilika na wanafunzi wanavutiwa zaidi na mazingira ya chuo,” amesema.
Ameongeza kuwa hapo awali gharama za kufika chuoni zilikuwa kubwa na wale waliokuwa wakitembea kwa miguu walikumbana na changamoto ya vumbi, lakini sasa wanafunzi na watumishi wanatumia barabara ya lami hali inayorahisisha shughuli zao za kila siku.
Ameongeza kusema uwepo wa barabara hiyo pia utafungua fursa za kiuchumi na uwekezaji katika eneo hilo pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya chuo na wadau mbalimbali wa maendeleo katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Taasisi hiyo iliyoanzishwa mwaka 1963 ina zaidi ya wanafunzi 4,000 na watumishi 240 ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakitumia barabara hiyo.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Chuo cha Mafunzo ya Mifugo Tengeru, Mwl. Hoshimu Mollel, amesema barabara hiyo ndiyo njia kuu ya kuingia na kutoka katika chuo hicho na kwa muda mrefu imekuwa changamoto kwa watumiaji.
Amesema kukamilika kwa barabara hiyo kumetoa matumaini mapya kwa taasisi mbalimbali zilizopo katika eneo hilo pamoja na wakulima wanaozunguka eneo hilo.
Ameongeza kuwa wana imani serikali itaendelea kuboresha miundombinu hiyo hadi kufika maeneo ya chini ambako kuna taasisi zaidi ya kumi pamoja na wakulima wengi watakaonufaika kwa kusafirisha mazao yao kwa urahisi.
