Featured Kitaifa

MWENYEKITI WA KAMATI YA TEITI ATEMBELEA MGODI WA DHAHABU WA GEITA, AAHIDI USHIRIKIANO NA WADAU WOTE

Written by Alex Sonna

 

📍*Geita.*

Mwenyekiti wa Kamati ya TEITI, Balozi Wilson Masilingi, ametembelea Mgodi wa Dhahabu wa Geita Gold Mining Limited akiambatana na Menejimenti ya TEITI, kwa lengo la kujitambulisha na kufanya mazungumzo na menejimenti ya mgodi huo.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Balozi Masilingi alisema ziara hiyo imelenga kujenga na kuimarisha ushirikiano kati ya TEITI na wadau wa sekta ya uziduaji, hususan migodi mikubwa inayochangia maendeleo ya taifa.

Alisema kuwa aliteuliwa kusimamia taasisi hiyo muhimu na Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan, Rais wa Tanzania, mwezi Januari mwaka huu, hivyo anaona ni muhimu kujitambulisha kwa wadau wakuu wa sekta hiyo ili kuimarisha ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu ya TEITI.

“Utekelezaji wa shughuli za EITI nchini ni wa ushirikiano, hivyo nitashirikiana kikamilifu na wadau wote ili kuendeleza gurudumu la uwazi na uwajibikaji katika sekta ya uziduaji,” alisema Balozi Masilingi.

Katika ziara hiyo, menejimenti ya mgodi ilitoa maelezo kuhusu maendeleo yaliyofikiwa tangu kuanzishwa kwa mgodi huo, ikiwemo namna wanavyotekeleza sheria, kanuni na miongozo ya sekta ya madini pamoja na masharti ya leseni ya uchimbaji.

Aidha, ilielezwa kuwa mgodi huo umeendelea kutenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) katika halmashauri mbalimbali za Mkoa wa Geita, hatua inayochangia maendeleo ya jamii zinazouzunguka mgodi.

Pia ilibainishwa kuwa kwa sasa mgodi huo unaendeshwa kwa kiasi kikubwa na Watanzania na umeendelea kuongeza ajira kwa wananchi wa ndani ikilinganishwa na miaka ya awali ya uendeshaji wake.

Balozi Masilingi aliishukuru menejimenti ya mgodi kwa mapokezi mazuri waliompatia pamoja na utayari wao wa kuendeleza ushirikiano kwa manufaa ya sekta ya uziduaji na maendeleo ya taifa.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa TEITI, Bi. Mariam Mgaya, aliishukuru menejimenti ya mgodi kwa kuendelea kushirikiana na TEITI katika utekelezaji wa matakwa ya EITI pamoja na Sheria ya TEITA ya mwaka 2015, inayolenga kuimarisha uwazi na uwajibikaji katika sekta ya uziduaji.

Alisisitiza kuwa ushirikiano huo unapaswa kuendelezwa ili kuongeza uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa rasilimali za madini, mafuta na gesi asilia nchini.

Naye Meneja wa mgodi huo, Bw. Ashraf Suryaningrat, alisema Geita Gold Mining Limited itaendelea kushirikiana kikamilifu na TEITI katika kufanikisha lengo la uwazi na uwajibikaji katika sekta ya uziduaji, akibainisha kuwa mgodi huo ni miongoni mwa wadau wakubwa wa TEITI nchini.

About the author

Alex Sonna