Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Hassan Abbas akifungua Mafunzo ya tasnia ya Filamu kwa Wasanii Chipukizi (Upcoming Film Stars) yanayoendeshwa na Ofisi ya Bodi ya Filamu Tanzania Kivukoni Jijini Dar es Salam
Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Dkt. Kiagho Kilonzo akieleza malengo ya mafunzo kwa Wasanii Chipukizi katika kuboresha na kukuza kazi za tasnia hiyo nchini.
Meneja Uhusiano Airtel Tanzania Bw. Jackson Mbando akielezea jambo wakati wa Mafunzo kwa Wasanii Chipukizi yaliyofanyika katika Ofisi za Bodi ya Filamu, Jijini Dar es Salaam.
…………………………………………………..
Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Hassan Abbas amewataka Wasanii Chipukizi katika Tasnia ya Filamu kufanya kazi kwa bidii na malengo dhabiti ili kufikia mafanikio makubwa ya ndoto zao katika Tasnia ya Filamu.
Hayo yameelezwa wakati wa akifungua Semina kwa Wasanii Chipukizi wa Filamu (Upcoming Film Stars) iliyoandaliwa na kufanyika katika Ofisi za Bodi ya Filamu Tanzania Juni 02,2022 Jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu Dkt. Abbas amewataka Wasanii hao kutokata tamaa pale wanapokutana na changamoto mbalimbalimbali za kiutendaji bali wahakikishe wanafanya kazi kwa bidii na kuzingatia maadili ili kukuza vipaji vyao na hatimaye wafikie mafanikio wanayohitaji. Ameongeza kuwa kwa kufanya hivyo tasnia ya Filamu itakuwa na wataweza kukuza Ajira na vipato binafsi na tija kwa Taifa.
“Safari ya kuelekea ndoto zenu inaweza kuwa na changamoto lakini pigania ufikie kile unachohitaji na unapohitaji kufikia katika tasnia ili siku moja utoke kuwa chipukizi uwe mtu maarufu katika tasnia ya Filamu,” alisema Dkt. Abbas
Aidha, amesema Serikali tayari inaendelea na jitihada kubwa za kuhakikisha Sanaa nchini inakuwa kwa kasi kwa kuhakikisha inaweka mazingira mazuri na miundombinu yatakayoleta mageuzi chanya na makubwa kukuza Sanaa. Sambamba na hilo amesema tayari taratibu za kuanzisha Mfuko wa Sanaa unaendelea hivyo Wadau wa Sanaa wawe tayari kushirikiana kwa kufanya kazi bora zitakazokuza Sanaa na kuitangaza vyema Tanzania.
Katibu Mkuu amewataka Wasanii hao kuhakikisha wanatayarisha kazi zao kwa kuzingatia maadili yanayokubalika na Jamii zetu ili kazi hizo zikawe sehemu ya kujenga maadili mema. Ameongeza Wasanii kuishi kwa maadili ili kutunza heshima ya tasnia na maisha binafsi.
Katika Ufunguzi huo Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Dkt. Kiagho Kilonzo amesema Bodi inaendesha mafunzo hayo kwa lengo la kuwajengea misingi bora ya kazi Wasanii Chipukizi wa Filamu ili kuwawezesha kuendeleza taswira chanya ya tasnia na kazi zao. Ameongeza kuwa Bodi imeanzisha Programu hiyo ambapo itakuwa ikikutana na Wasanii Chipukizi kila mwezi kuwajengea uwezo utakaosaidia kuboresha kazi zao na kukuza soko la Filamu.
Kwa upande wake Muigizaji Chipukizi Catherine Krido ameshukuru kwa fursa ya mafunzo hayo kwakuwa ni fursa kwao kujifunza mengi kuhusu tasnia ya Filamu pamoja na kufahamiana, kubadilishan uzoefu jambo ambalo litawasaidia kuwa na ushirikiano wa pamojaa katika kazi zao.