Meya wa Jiji la Arusha Maximilian Iranqe akiongea wakati wa uzinduzi wa kampeni ya uwekaji mipaka katika hifadhi za vyanzo vya maji Jiji la Arusha.
Mkurugenzi wa bodi ya maji ya bonde la mto Pangani Segule Segule akiongea na waandishi wa habari katika uzinduzi wa kampeni ya uwekaji mipaka katika hifadhi za vyanzo vya maji.
Meya wa Jiji la Arusha Maximilian Iranqe akishirikiana na Mkurugenzi wa bodi ya maji ya bonde la mto Pangani Segule Segule kuzindua kampeni ya uwekaji mipaka katika hifadhi za vyanzo vya maji Jiji la Arusha
……………………………………………
NA NAMNYAK KIVUYO, ARUSHA
Bodi ya maji ya bonde la mto Pangani imezindua kampeni la uwekaji wa mipaka katika hifadhi ya vyanzo vya maji ili kuhakikisha vyanzo hivyo vinakua endelevu pamoja na kuzuia watu kufanya shughuli za kibinadamu ikiwemo ujenzi katika vyanzo hivyo.
Aidha kuutokana na ongezeko la makazi holela katika vyanzo vya maji jijini Arusha Meya jiji la Arusha Maximilian Iranqe amewataka maofisa wa mipango miji kujitathmini juu ya utoaji vibali vya ujenzi katika maeneo ya hifadhi ya vyanzo vya maji ndani ya mita 60.
Meya alitoa rai hiyo wakati akizungumza katika uzinduzi wa kampeni hiyo ambapo alisema kuwa anawashangaa maafisa mipango miji kutoa vibali vya ujenzi katika hifadhi ya mito huku wakijua na kinyume na sheria ya utunzaji wa vyanzo hivyo, hivyo ni vyema wakajitafakari.
“Kupitia hilo napenda kutoa rahi kwa wananchi wa jiji la Arusha kuhakikisha wanatunza mazingira katika vyanzo vya maji na kuendesha shughuli za kibinadamu pembezoni mwa mito ndani ya mita 60 ni kinyume na sheria,”alisema Meya.
Alisema kupitia zoezi hilo la uwekaji wa alama ni kuwajulisha ujenzi walioufanya ndani ya mita 60 sio mahali sahihi na mito inayoongoza kwa makazi ya watu ni mto Ngarenaro,Kijenge na Themi hivyo ni vyema wadau wa mazingira wakawekeza elimu katika maeneo hayo.
Akiendelea kusema kuwa pamoja na bonde la Pangani kuweka alama hizo kwa ajili ya kuwajulisha wananchi maeneo ya hifadhi ya mito ambayo hairuhusiwi pia halmashauri ya jiji la Arusha wataongeza beaconi kwa ajili ya kumalizia zoezi hilo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa bodi ya maji bonde la mto Pangani,Segule Segule alisema ili kuhakikisha vyanzo vya maji vinakuwa endelevu ni lazima kuanzia katika vyanzo husika na kusimamia kwa lengo la kuhakikisha hayaleti madhara kwa watu.
“Maji pia yasipotumika vyema yanaweza kuwa ni silaha mbaya kwa binadamu na kutokana na vyanzo hivho kuwepo katika sehemu mbalimbali ushiriki wa wadau ni muhimu sana ni vyema kila mmoja akatekeleza wajibu wake katika nafasi yake katika maeneo mbalimbali,”alisema.
Segule Segule alisema zoezi hilo la uwekaji alama limeanza katika mto Naura lengo ni pamoja na kuhamasisha utunzaji wa vyanzo vya maji ikiwa shughuli za binadamu zinatakiwa kufanyika nje ya mita 60 kingo za vyanzo.
Kwa upande wake Afisa mazingira kutoka bodi ya maji bonde la mto Pangani,Felista Joseph alisema changamoto zilizopo katika mto Naura ni pamoja na shughuli za kibinadamu,ujenzi wa makazi ya watu katika eneo la chanzo cha mto Naura na utupaji wa taka ngumu.
“Shughuli mbalimbali za biandamu zimekuwa zikiathiri ubora wa maji hivyo uwekaji wa alama hizo zitakwenda kuondoa baadhi ya changamoto hizo ili yeyote anapokiuka sheria apate adhabu kwa mujibu wa kanuni,”Alisema.