Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa akizungumza wakati akimkaribisha Naibu Waziri wa Madini wa Zimbabwe na Ujumbe wake wakati wa ziara yenye lengo la kujifunza masuala mbalimbali ya usimamizi wa Sekta ya Madini
Naibu Waziri wa Madini wa Zimbabwe Dkt. Mhandisi Polite Kambamura akizungumza mara baada ya kutembelea kiwanda cha kusafisha dhahabu cha Mwanza ili kujifunza masuala mbalimbali ya usimamizi wa Sekta ya Madini Jijini Mwanza
Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa na akiwa na Naibu Waziri wa Madini wa Zimbabwe na Ujumbe wake wakiwa kwenye kiwanda cha kusafisha dhahabu cha Mwanza ili kujifunza masuala mbalimbali ya usimamizi wa Sekta ya Madini Jijini Mwanza.
……………………………………………
IMEELEZWA kuwa, ziara ya Naibu Waziri wa Madini wa Zimbabwe na wataalamu wake imelenga katika kujengeana uwezo kuhusu Sekta ya Madini inavyofanya kazi hapa nchini ili kujifunza masuala mbalimbali ya usimamizi katika sekta hiyo.
Hayo yamebainishwa leo Mei 23, 2022 na Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa wakati akimkaribisha Naibu Waziri wa Madini wa Zimbabwe, Dkt. Mhandisi Polite Kambamura na ujumbe wake Mkoani Mwanza, kujifunza namna bora ya uchimbaji, utafutaji, uongezaji thamani na biashara ya madini.
Akizungumza, katika kiwanda cha kusafisha dhahabu cha Mwanza (Mwanza Precious Metals Refinery Company Limited),Dkt.Kiruswa amesema, ushirikiano wa Tanzania na Zimbabwe kwenye Sekta ya Madini ni wa kujengeana uwezo kwa kuwa Zimbabwe imepiga hatua kubwa kwenye sekta ya madini kupitia wawekezaji wakubwa.
Amesema, ujumbe wa Sekta ya Madini kutoka Zimbabwe unataka kujifunza namna gani Tanzania imefanikiwa katika kuwalea wachimbaji wadogo hadi kufanikiwa kuwatengenezea masoko ya madini ya kuuza na kununua hapa nchini.
Amesema ujumbe huo, utajifunza kuhusu fursa ya madini yaliyopo Tanzania, mfumo wa usimamizi wa leseni na usimamizi wa wachimbaji wadogo.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini wa Zimbabwe, Dkt. Mhandisi Kambamura amevutiwa na kiwanda cha kusafisha dhahabu cha Mwanza ambacho kinasafisha kiasi cha kilo 480 za dhahabu kwa siku kwa ubora wa asilimia 999.9.
Amesema, Tanzania ni nchi iliyofanikiwa kwenye Sekta ya Madini hususan kuwaendeleza wachimbaji wadogo jambo lililofanya waje kujifunza.
Naye, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala, Deusdedith Magala akizungumza kwa niaba ya STAMICO amesema, kiwanda cha kusafisha dhahabu nchini itafanya wafanyabiashara wa Zinbabwe wavutiwe kupeleka dhahabu yao kwa ajili ya kusafishwa katika kiwanda cha Mwanza kutokana na kuwepo kwa mazingira wenzeshi ya uwekezaji hapa nchini.
Naibu Waziri wa Madini Zimbabwe na ujumbe wake wapo nchini kwa ziara ya siku tano. Katika ziara hiyo watatembelea mgodi wa dhahabu wa GGM, wachimbaji wadogo wa Nyarugusu na wachimbaji wadogo wa almasi wa Shinyanga.