Featured Kitaifa

WMA YAWATAKA WANANCHI KUNUNUA MCHANGA NA KOKOTO KWA MITA ZA UJAZO

Written by Alex Sonna

Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo (WMA), Alban Kihulla, akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu utekelezaji mwaka wa fedha 2025/2026 na mwelekeo wa wakala huo  kwa mwaka 2026/2027, leo Septemba 18, 2026 katika ukumbi wa Idara ya Habari – MAELEZO uliopo jengo la Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dodoma.

Na.Alex Sonna,Mzalendo blog-DODOMA

WANANCHI wanaojenga nyumba wametakiwa kuacha kutumia ‘tripu’ za lori kama kipimo cha kununulia mchanga, kokoto, vifusi vya udongo na mawe, badala yake watumie kipimo cha mita za ujazo (cubic metre) ili kupata kiasi sahihi cha vifaa wanavyolipia.

Ushauri huo umetolewa leo Septemba 18,2026 jijini Dodoma na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA), Alban Kihula, wakati akitoa taarifa kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Wakala kwa mwaka wa fedha 2025/2026 pamoja na mwelekeo wa mwaka 2027.

Kihula amesema matumizi ya ‘tripu’ ya lori si kipimo rasmi kwa kuwa kiasi cha bidhaa kinachobebwa kinaweza kutofautiana kutokana na ukubwa na ujazo wa lori, hali inayoweza kumfanya mnunuzi kupata kiasi kisicholingana na fedha alizolipa.

Amesema WMA imeendelea kusimamia usahihi wa vipimo vinavyotumika katika biashara ya bidhaa hizo, ambapo hadi sasa Wakala imehakiki zaidi ya malori 27,000 yanayotumika kusafirisha mchanga, kokoto, vifusi vya udongo na mawe.

Katika hatua nyingine, Kihula amewataka wananchi kuacha kutumia madebe, makopo, visado na mafungu kama vipimo katika ununuzi wa bidhaa, akisema vipimo hivyo havina kiwango kinachofanana na matumizi yake yanakiuka matakwa ya Sheria ya Vipimo.

“Madebe, makopo, visado na mafungu sio kipimo na ni kinyume na sheria, hili ni kosa la jinai,” amesema Kihula.

Amesema wananchi wanapaswa kujenga utamaduni wa kutumia mizani wakati wa kununua bidhaa zinazouzwa kwa uzito, ikiwemo nyanya na vitunguu, ili kuhakikisha kiasi wanachopata kinaendana na fedha wanazolipa.

“Niwasihi wafanyabiashara kununua mizani kupima mazao kama nyanya na vitunguu kwa kutumia mizani na sisi wananchi tupende kununua vitu kwenye mizani,” amesema.

Kihula amesema matumizi ya vipimo sahihi yana umuhimu mkubwa katika kulinda maslahi ya wanunuzi na wafanyabiashara, kwani huongeza uwazi katika biashara na kuhakikisha kila upande anapata haki kulingana na kiasi cha bidhaa kilichopimwa.

Akizungumzia utekelezaji wa majukumu ya WMA, Kihula amesema katika mwaka wa fedha 2025/2026, Wakala ilihakiki vipimo milioni 1.1 kati ya lengo la vipimo milioni 1.2, sawa na asilimia 92 ya lengo lililowekwa.

Amesema hatua hizo ni sehemu ya juhudi za WMA kuhakikisha matumizi ya vipimo sahihi yanaimarishwa katika maeneo mbalimbali ya biashara nchini, kwa lengo la kulinda mlaji na kuongeza uaminifu katika shughuli za kiuchumi.

About the author

Alex Sonna