Na Mwandishi Wetu – Ruangwa, Lindi.
Serikali yawahimiza wachimbaji wa Madini kutumia teknolojia za kisasa katika shughuli za uchimbaji ili kuhakikisha wanachimba kwa faida, kuongeza tija katika Sekta ya Madini na kuchangia maendeleo ya Taifa kwa ujumla.
Wito huo umetolewa leo, Septemba 18, 2026, na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe.Kaspar Mmuya
Mmuya, wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya Madini Mkoa wa Lindi kwa mwaka 2026, yaliyofanyika wilayani Ruangwa kwa lengo la kutangaza fursa za Madini zilizopo katika mkoa huo, ambapo amesisitiza umuhimu wa wachimbaji kutumia teknolojia za kisasa katika shughuli zao ili kuongeza ufanisi na kupata tija zaidi.
Alizungumzia uongezaji thamani wa Madini kupitia viwanda vya uchenjuaji katika maeneo yanapozalishwa madini utawasaidia wachimbaji kupata faida zaidi, huku kuongeza ushindani wa Madini katika soko.
“Tutumie teknolojia ya kisasa katika kazi zetu za uchimbaji wa madini ili tuchimbe kwa faida. Naomba kuwe na viwanda vya uchenjuaji wa Madini ambavyo vitakuwa vinaongeza thamani ya madini katika maeneo husika ya wachimbaji,” amesema Mhe. Mmuya.
Pia, Mhe. Mmuya amewasisitiza wachimbaji wadogo wa Madini kuwa na malengo na dira kubwa zitakazowawezesha kukua na kuwa wachimbaji wakubwa ili kumiliki viwanda
Sambamba na hayo, Mhe. Mmuya ametaka maonesho hayo yatumike kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo katika Mkoa wa Lindi, huku akiwataka wawekezaji kutoka maeneo mbalimbali kwenda kuwekeza mkoani humo kutokana na uwepo wa aina mbalimbali za Madini.
“Nayataka maonesho haya yatumike kutangaza fursa za uwekezaji wa madini katika Mkoa wa Lindi. Na wawekezaji njooni muwekeze hapa, kuna Madini mengi sana,” amesema Mhe. Mmuya.
Aidha, amewahamasisha wananchi wa Mkoa wa Lindi kushiriki katika shughuli za Madini, akisema sera za nchi zinataka wazawa wa maeneo husika kunufaika na shughuli za uchimbaji wa Madini katika maeneo yao.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini, Mhe. Dkt. Steven Kiruswa, amesema Wizara ya Madini imejipanga kufanya utafiti wa Madini nchini kote kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), ili kuhakikisha wachimbaji wanafanya shughuli zao katika maeneo yenye uhakika wa uwepo wa m
Madini.
“Tumejipanga Wizara ya Madini kuwasaidia wachimbaji kwa kufanya utafiti wa Madini nchi nzima kupitia GST, na Mhe. Rais tayari ameshatoa fedha za kufanya utafiti huo,” amesema Dkt. Kiruswa.
Dkt. Kiruswa amewataka Watanzania kuendelea kuomba leseni za uchimbaji wa Madini, akisema Wizara ya Madini inaendelea kufuta leseni za uchimbaji ambazo hazijaendelezwa ili kuwapa fursa watu wengine wenye nia ya kuwekeza katika Sekta ya Madini.
Pia, amesema Wizara ya Madini imeanzisha programu maalumu ya “Mining For A Better Tomorrow”, inayolenga kuwawezesha makundi mbalimbali, ikiwemo vijana, watu wenye mahitaji maalum na wanawake, kushiriki na kunufaika katika Sekta ya Madini.
Naye, mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Lindi, ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Liwale, Goodluck Mlinga, amesema maonesho hayo yana umuhimu mkubwa katika kuwaelimisha na kuwahamasisha wananchi kushiriki katika shughuli za uchimbaji wa Madini.