Na WMJJWM, Arusha
Wadau wanaotekeleza Afua za vijana balehe wametakiwa kushirikisha vijana katika uandaaji na utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Afya na Maendeleo ya Vijana Balehe (PJT–AMAVIBA: 2026/27–
2030/31)
Agizo hilo limetolewa na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amon Mpanju wakati akifungua kikao cha kwanza cha wadau kwa lengo la kuandaa Programu hiyo ya Kitaifa, kinachofanyika mkoani Arusha kwa siku mbili Septemba 16-17, 2026.
Mpanju amehimiza kuwa, Programu hiyo mpya inayopendekezwa, inalenga kuweka mwelekeo wa pamoja wa kitaifa katika kushughulikia masuala ya afya na maendeleo ya vijana balehe kwa kuunganisha juhudi za Serikali kupitia Wizara, Idara na Taasisi, Wadau wa Maendeleo, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Taasisi za Kitaaluma, Sekta Binafsi na wadau wengine.
“Mabadiliko haya ya kimfumo kutoka Ajenda ya ya Kitaifa ya Kuwekeza katika Afya na Maendeleo ya Vijana Balehe (NAIA) kwenda Programu Kamili ya Kitaifa yanalenga kuimarisha na kupanua mafanikio ya awamu ya kwanza hususan katika utoaji wa huduma rafiki kwa vijana balehe katika maeneo ambayo awali hayakuwa na mazingira bora.” amesema Wakili Mpanju.
Aidha, Wakili Mpanju amesema programu hiyo inahusisha sekta zote katika kumuendeleza na kumuandaa kijana na kumpa uwezo wa kupata kipato ili kuchangia maendeleo ya Taifa huku akisistiza makundi yote kwenye jamii lazima yajumuishwe hususani Vijana wenyewe, Wazazi, Viongozi wa Dini na Wizara zote.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya watoto, Malezi na Familia Asha Shame Vuai amebainisha kwamba, lengo la kikao hicho ni kujadili namna ya kuandaa Programu hiyo hasa kuimarisha ubora na umiliki wa pamoja wa nyaraka za maandalizi yake kabla ya kukamilishwa kwake.
Naye mmoja wa vijana aliyeshiriki kikao hicho Neema Mtavangu amesema vijana balehe bado wanakabiliwa na changamoto ya maambukizi ya VVU, hivyo ameomba Serikali na wadau wazidi kuwashirikisha ili kuwasaidia kujitambua na kujiepusha na changamoto mbalimbali.
Kikao hicho ni hatua muhimu katika mchakato wa kuandaa Programu Jumuishi ya Taifa ya Afya na Maendeleo ya Vijana Balehe (PJT–AMAVIBA: 2026/27–
2030/31) ikiwa ni utekelezaji wa mapendekezo ya Tathmini ya iliyofanyika
katika Ajenda ya Kitaifa ya Kuwekeza katika Afya na Ustawi wa vijana ya mwaka 2021- 2025 (NAIA-AHW).
