Featured Kitaifa

MAKAMU WA RAIS AAGIZA DAMPO LA PUGU KUBORESHWA HARAKA

Written by Alex Sonna

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam na Halmashauri zake kuhakikisha hali ya Dampo la Pugu inaboreshwa, huku akielekeza maeneo ya makazi yanayozunguka dampo hilo kupuliziwa dawa ili kuwalinda wananchi dhidi ya wadudu na kupunguza hatari ya magonjwa, hususan katika kipindi cha mvua.

Makamu wa Rais ametoa maelekezo hayo leo, Septemba 18, 2026, alipofanya ziara katika Dampo la Pugu linalotumika kukusanya taka za Mkoa wa Dar es Salaam ili kujionea hali halisi ya eneo hilo na kusikiliza kero za wananchi wanaoishi maeneo ya jirani.

Aidha, ameelekeza kuandaliwa kwa mpango kazi wa pamoja utakaoainisha hatua za haraka na za muda mrefu za kukabiliana na changamoto za uendeshaji wa Dampo la Pugu pamoja na kero zinazowakabili wananchi wanaoishi katika maeneo yanayolizunguka, ikiwemo kutopuliziwa dawa za kuua wadudu.

Akiwa katika dampo hilo, Mhe. Ndejembi ameonesha kutoridhishwa na kutofautiana kwa takwimu kuhusu kiasi cha taka zinazokusanywa na kupelekwa katika Dampo la Pugu kila siku kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dar es Salaam.

Kutokana na hali hiyo, amezitaka mamlaka zote zinazohusika kukaa pamoja, kuhakiki na kuweka takwimu sahihi zitakazokuwa msingi wa kupanga na kutekeleza hatua madhubuti za kuboresha usimamizi wa taka jijini Dar es Salaam.

“Hatuwezi kutatua changamoto za eneo hili bila kuwa na taarifa na takwimu sahihi. Hawa wananchi mnaowaona wamechoka na stori; wanataka kuona kazi,” alisisitiza Makamu wa Rais.

Makamu wa Rais amesema wananchi wanatarajia kuona matokeo ya moja kwa moja ya hatua zinazochukuliwa na Serikali, hivyo amewataka viongozi na taasisi husika kuharakisha utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha kero za wananchi zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Makamu wa Rais amesema Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni Serikali sikivu inayojali maslahi ya Watanzania na itahakikisha changamoto za watanzania zinatatuliwa kwa wakati.

Katika hatua nyingine, Mhe. Ndejembi ametoa siku saba kwa mawaziri wanaohusika na TAMISEMI, Maliasili na Utalii pamoja na Ardhi kufika katika maeneo husika na kutatua mgogoro wa muda mrefu unaohusu mipaka ya kiutawala na mpaka wa Msitu wa Kazimzumbwi, ambao umekuwa ukiwaathiri wananchi wa Pugu na maeneo ya jirani.

Changamoto hiyo imesababisha baadhi ya wananchi kutokuwa na uhakika kuhusu maeneo yao ya makazi kutokana na kutofahamika kwa mipaka ya kiutawala pamoja na mpaka wa Msitu wa Kazimzumbwi.

Makamu wa Rais ameelekeza mawaziri hao kufika wenyewe katika maeneo yenye mgogoro na, kwa kushirikiana na wananchi pamoja na wataalamu, kusoma ramani na matangazo rasmi ya Serikali (GN) ili kuweka wazi mipaka na kuwawezesha wananchi kutambua kwa uhakika maeneo yao.

“Waheshimiwa Mawaziri, nataka mfike wenyewe kwenye eneo hili kutambua GN za mikoa na mipaka ya Msitu wa Kazimzumbwi, kwani hii imekuwa kero ya muda mrefu. Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, anataka tutatue kero za wananchi; kwa hiyo naelekeza hili mkalifanyie kazi ndani ya siku saba liwe limeisha,” alisema Mhe. Ndejembi.

Awali, wananchi wa maeneo ya Mstafa, Viwege na Kinyamwezi walitumia fursa ya ziara hiyo kueleza changamoto mbalimbali zinazowakabili, zikiwemo athari zinazotokana na uwepo wa dampo, kutopuliziwa dawa za kuua wadudu katika maeneo yao, ukosefu wa maji kwa muda mrefu pamoja na migogoro ya ardhi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, ameahidi kusimamia kikamilifu utekelezaji wa maelekezo yote yaliyotolewa na Makamu wa Rais.

Miongoni mwa hatua zitakazotekelezwa ni kuboresha usimamizi wa Dampo la Pugu, kuweka utaratibu wa kila Halmashauri kutenga bajeti mahsusi kwa ajili ya uendeshaji wa dampo hilo, pamoja na kuimarisha upatikanaji wa vifaa na kuboresha miundombinu muhimu ili shughuli za dampo ziendeshwe kwa kuzingatia matakwa ya kimazingira na kiafya.

Hatua hizo zinalenga kuimarisha usimamizi wa taka katika Mkoa wa Dar es Salaam na kuhakikisha changamoto za mazingira, afya na mipaka ya ardhi zinazowakabili wananchi wa Pugu na maeneo ya jirani zinapatiwa ufumbuzi wa haraka na wa kudumu.

Katika ziara hiyo, Makamu wa Rais ameambatana na viongozi mbalimbali wa Serikali, akiwemo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI Mhe. Prof Riziki Shemdoe, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Masauni, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Reuben Kwagilwa, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, Wakuu wa Wilaya pamoja na viongozi kutoka Halmashauri za Mkoa wa Dar es Salaam.

    

About the author

Alex Sonna