Na WMA – DODOMA
WAKALA wa Vipimo (WMA) umewataka wafanyabiashara na wananchi kuacha mara moja matumizi ya vipimo visivyo rasmi, ikiwemo ndoo, mafungu, visado na makopo, katika uuzaji wa mazao ya kilimo na mifugo na badala yake kutumia mizani iliyohakikiwa kwa mujibu wa sheria.
Wito huo umetolewa na Afisa Mtendaji Mkuu wa WMA, Alban Kihula, leo Agosti 8, 2026 wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya 33 ya Kitaifa ya Siku ya Wakulima Nane Nane, yaliyokuwa yakifanyika katika Viwanja vya Dkt. John Samwel Malecela, jijini Dodoma.
Kihula amesema matumizi ya vipimo visivyo rasmi yanaweza kusababisha kutokuwepo kwa usawa katika biashara na kuwaathiri wananchi kwa kuwafanya wasipate thamani halisi ya bidhaa wanazonunua au kuuza.
Amesema WMA imeendelea kutoa elimu kwa wananchi, wakulima, wafugaji na wafanyabiashara kuhusu matakwa ya Sheria ya Vipimo, Sura ya 340, ikiwemo namna ya kutambua vipimo vilivyohakikiwa na uwekaji wa alama sahihi kwenye bidhaa zilizofungashwa.
“Ili kuwa na soko lenye haki na kuongeza tija kuelekea Dira ya 2050, hakuna soko linaloweza kuwa la haki bila matumizi ya vipimo vilivyohakikiwa kwa mujibu wa sheria,” amesema Kihula.
Akizungumzia sekta ya kilimo, Kihula amewataka wakulima kuzingatia matumizi ya vipimo sahihi katika hatua zote za uzalishaji na biashara, kuanzia uandaaji wa mashamba hadi uvunaji, uhifadhi na uuzaji wa mazao.
Amesema matumizi ya vipimo sahihi katika kujua ukubwa wa eneo la shamba yanaweza kusaidia wakulima kupanga uzalishaji kwa usahihi badala ya kutegemea makadirio.
Aidha, amewataka kuhakikisha mazao yanapimwa kwa mizani iliyohakikiwa wakati wa kuuza ili mkulima aweze kupata thamani halisi ya bidhaa zake.
Kwa upande wa wafugaji, Kihula amewataka kuacha kuuza mifugo kwa kutegemea makadirio ya macho na badala yake kutumia mizani sahihi katika kubaini uzito wa mifugo kama vile ng’ombe, mbuzi, kondoo na kuku.
Amesema utaratibu huo unapaswa pia kuzingatiwa katika uuzaji wa bidhaa zinazotokana na mifugo, ikiwemo nyama na maziwa, ili kuhakikisha mnunuzi na muuzaji wanapata thamani inayolingana na kiasi cha bidhaa kinachouzwa.
Wakati huohuo, Kihula amewapongeza wavuvi kwa kuendelea kuonesha mfano mzuri katika matumizi ya vipimo na kuwataka kuendeleza utaratibu huo.
Amesema matumizi ya vipimo sahihi katika shughuli za uvuvi ni muhimu katika kuhakikisha biashara inafanyika kwa uwazi na kwa kuzingatia thamani halisi ya bidhaa.
Kihula amewataka wananchi kuwa mstari wa mbele kukataa kuhudumiwa kwa vipimo visivyo rasmi wanaponunua bidhaa kama vile viazi, bamia, vitunguu na nyanya, badala yake kusisitiza bidhaa hizo zipimwe kwa mizani iliyohakikiwa.
“Wananchi wasikubali kununua bidhaa kwa mafungu, visado au vipimo vingine visivyo rasmi. Wanapaswa kusisitiza kupimiwa kwa mizani iliyohakikiwa ili kuhakikisha wanapata kiasi sahihi cha bidhaa wanacholipia,” amesema.
Aidha, amewataka wananchi kutoa taarifa kwa WMA wanapobaini matumizi ya vipimo visivyo halali katika maeneo yao ili hatua stahiki za kisheria ziweze kuchukuliwa.
Amesema ushirikiano wa wananchi, wafanyabiashara na taasisi za Serikali ni muhimu katika kujenga soko lenye haki, uwazi na linalozingatia matumizi ya vipimo sahihi kwa mujibu wa sheria.
Amesisitiza kuwa matumizi ya vipimo vilivyohakikiwa si suala la wafanyabiashara pekee, bali ni jambo linalomhusu kila mwananchi katika kuhakikisha anapata thamani halisi ya fedha anayolipa au mapato anayopata kutokana na bidhaa anazouza.
