Featured Kitaifa

TUNATAMANI KUWA MABALOZI WA VIPIMO – WANAFUNZI MWANZA

Written by Alex Sonna

 

 

*Mwanafunzi Ibrahim Omary, kutoka Shule ya Msingi Ghana jijini Mwanza, akipokea zawadi kutoka kwa Meneja Mawasiliano wa Wakala wa Vipimo (WMA), Bi. Veronica Simba baada ya kutoa elimu ya vipimo kwa ustadi kwa wananchi waliotembelea banda la WMA katika siku ya pili ya Maonesho ya Biashara ya Afrika Mashariki yanayoendelea jijini Mwanza, Agosti 29, 2026.*

*Mwanafunzi Ibrahim Omary, kutoka Shule ya Msingi Ghana iliyopo jijini Mwanza, akitoa elimu ya vipimo kwa wanafunzi wenzake waliotembelea banda la Wakala wa Vipimo (WMA) katika siku ya pili ya Maonesho ya Biashara ya Afrika Mashariki yanayoendelea katika Viwanja vya Furahisha jijini Mwanza, Agosti 29, 2026.*

*Meneja wa Wakala wa Vipimo (WMA) Mkoa wa Mwanza, Bw. Karim Zuberi akitoa elimu ya vipimo kwa mmoja wa wajasiriamali aliyetembelea Banda la WMA katika siku ya pili ya Maonesho ya Biashara ya Afrika Mashariki yanayoendelea katika Viwanja vya Furahisha jijini Mwanza, Agosti 29, 2026.*

*Wananchi mbalimbali wakipata elimu ya vipimo katika Banda la Wakala wa Vipimo (WMA) kwenye Maonesho ya Biashara ya Afrika Mashariki yanayoendelea katika Viwanja vya Furahisha jijini Mwanza, Agosti 29, 2026.*

 Na WMA – Mwanza

Wanafunzi kutoka shule mbalimbali za Msingi na Sekondari jijini Mwanza wameomba Wakala wa Vipimo (WMA) kuanzisha Klabu za Vipimo katika shule za Mkoa huo.

Ombi hilo wamelitoa leo Jumamosi, Agosti 29, 2026 walipotembelea banda la WMA katika Maonesho ya Biashara ya Afrika Mashariki yanayoendelea viwanja vya Furahisha, Jijini Mwanza.

Ili kuthibitisha kiu yao ya elimu ya vipimo, mwanafunzi mmoja kutoka Shule ya Msingi Ghana, Ibrahim Omary, alijitolea na kupewa fursa ya kutoa elimu ya vipimo kwa wanafunzi wenzake na wananchi waliotembelea banda hilo. Aliifanya kazi hiyo kwa ufasaha mkubwa na kupata pongezi.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Ibrahim alisema: 

“Tuliona kwenye vyombo vya habari wanafunzi wenzetu jijini Dodoma ambao wako katika Klabu za Vipimo wakitoa elimu ya vipimo, tukavutiwa sana. Nasi tunaomba WMA waanzishe klabu hizo kwa shule za Mwanza ili nasi tupate elimu hiyo kwa kina.”

Wanafunzi hao wameahidi kuwa mabalozi wa WMA katika jamii zao kwa kuelimisha wenzao, familia na majirani kuhusu umuhimu wa matumizi sahihi ya vipimo. Wengi wao wamesema ndoto yao ni kuwa Maafisa Vipimo.

Akijibu ombi hilo, Meneja Mawasiliano wa WMA, Bi. Veronica Simba amewaahidi wanafunzi hao kuwa Wakala utaanzisha Klabu za Vipimo katika shule za Mkoa wa Mwanza na hatua kwa hatua katika mikoa mingine yote nchini.

“Lengo letu ni kufikisha elimu ya vipimo kwa watoto tangu awali. Kupitia klabu hizi tunajenga kizazi cha wafanyabiashara na watumiaji wanaojali haki na usawa katika biashara,” amesema Bi. Simba.

Wanafunzi na wananchi wengine wameendelea kufurika katika banda la WMA katika siku ya pili ya maonesho hayo. Wamesema wameridhishwa na elimu wanayopata kuhusu umuhimu wa matumizi sahihi ya vipimo.

Maonesho hayo yameanza tarehe 28 Agosti 2026 na yanahitimishwa tarehe 6 Septemba 2026 yakiwa na kaulimbiu “Usalama na Amani ni Kichocheo cha Biashara na Uwekezaji hapa Nchini”.  

Katika Maonesho hayo, WMA inatumia kaulimbiu isemayo “Vipimo Sahihi ni Msingi wa Usalama, Amani na Uwekezaji wa Biashara ”.

About the author

Alex Sonna