Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Udhibiti wa Mbegu za Kilimo Tanzania (TOSCI), Nyasebwa E. Chimagu,akizungumza katika Mkutano wa wadau wa kilimo ikolojia uliofanyika ndani ya Maonesho ya Kilimo ya Nanenane Kitaifa jijini Dodoma,
….
Taasisi ya Udhibiti wa Mbegu za Kilimo Tanzania (TOSCI) imeeleza kuwa ulinzi na usimamizi wa mbegu za asili ni nguzo muhimu katika kuhakikisha taifa linaendelea kuwa na usalama wa chakula, kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuhifadhi urithi wa rasilimali za mimea kwa vizazi vijavyo.
Akizungumza katika mkutano wa wadau wa kilimo ikolojia uliofanyika ndani ya Maonesho ya Kilimo ya Nanenane Kitaifa jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa TOSCI, Nyasebwa E. Chimagu, alisema mbegu za asili zinapaswa kuhifadhiwa kwa kufuata mifumo rasmi ya usimamizi ili kuhakikisha zinabaki salama, zenye ubora na zisizo na magonjwa yanayoweza kuhatarisha uzalishaji wa mazao.
Alisema pamoja na umuhimu wa mbegu hizo katika kuhifadhi bionuai na kuongeza uchaguzi kwa wakulima, sheria za mbegu nchini zinazitambua na kuzielekeza kupitia taratibu za usajili na uthibitishaji wa ubora kama ilivyo kwa mbegu nyingine zinazozalishwa kwa matumizi ya kibiashara. Aidha, alibainisha kuwa Serikali imeanza maandalizi ya kutunga sheria maalumu itakayotekeleza matakwa ya Mkataba wa Kimataifa wa mwaka 2001 kuhusu haki za wakulima na uhifadhi wa rasilimali za mimea.
Chimagu alisema ongezeko la watu pamoja na mabadiliko ya tabianchi vinaongeza umuhimu wa kuhifadhi nasaba za mimea, akieleza kuwa TOSCI kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo inaendelea kuwekeza katika tafiti za kuboresha mbegu na kuzifanya ziweze kustahimili mazingira yanayobadilika huku zikiendelea kutoa mazao yenye tija.
Aliongeza kuwa uzoefu kutoka mataifa mbalimbali unaonyesha mchango mkubwa wa matumizi ya mbegu bora katika kuongeza uzalishaji, akitolea mfano Misri ambako wakulima wa mahindi hufikia mavuno ya tani 10 hadi 12 kwa hekta kutokana na matumizi ya mbegu bora na teknolojia sahihi. Alisisitiza kuwa Tanzania inalenga kuwapa wakulima fursa ya kuchagua mbegu zinazokidhi mahitaji yao bila kupoteza hazina ya mbegu za asili.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mtandao wa Mashirika Yanayojishughulisha na Utunzaji wa Bionuai Tanzania (TABIO), Abdullah Ramadhan Mkindi, alisema juhudi za kuhifadhi mbegu za asili zinapaswa kwenda sambamba na uhifadhi wa mifugo ya asili ili kulinda bionuai, kuimarisha usalama wa chakula na kuhifadhi mazingira.
Naye Mratibu wa Utafiti na Masuala ya Kisera kutoka Swiss Aid Tanzania, Gladness Martine, alisema taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuimarisha tafiti shirikishi zitakazowawezesha wakulima kuhifadhi na kutumia mbegu za asili kwa tija ya kizazi cha sasa na kijacho.
